The House of Favourite Newspapers

Bilioni 1.2 Zamng’oa Michael Sarpong Yanga

0

DILI limefichuka rasmi kuwa Klabu ya Yanga ipo tayari kumuachia mshambuliaji wao, Michael Sarpong endapo tu kama kuna timu itakuwa tayari kulipa fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya kumsajili.

 

Sarpong mwenye uraia wa Ghana, alijiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Rayon Sports ya nchini Rwanda katika usajili wa dirisha kubwa msimu huu.

 

Chanzo chetu cha uhakika ndani ya Yanga, kililiambia Spoti Xtra kuwa kabla ya mshambuliaji huyo kuja Yanga alitakiwa kujiunga na moja ya klabu kutoka China kwa kiasi cha shilingi bilioni 1.5, lakini dili hilo liliharibika kutokana na uwepo wa janga la Corona, hivyo kama Wachina hao watamuhitaji tena, itabidi walipe shilingi bilioni 1.2.

“Sarpong kabla ya kusajiliwa na Yanga alikuwa akihitajika na timu nyingi ndani na nje ya Afrika, kuna timu kutoka China ilikuwa tayari kumsajili kwa fedha ndefu zisizopungua shilingi bilioni 1.5, lakini dili lao lilikwama kutokana na uwepo wa janga la corona, ila kama kusingekuwepo na janga hilo basi Sarpong angekuwa anakipiga Ligi ya China.

 

“Wachina hao bado hawajakata tamaa ya kumuhitaji Sarpong kwani wanamfuatilia kwa ajili ya kujaribu kumsajili tena, Yanga wanaweza kumuachia Sarpong lakini itawalazimu kumnunua mshambuliaji huyo kwa shilingi bilioni 1.2,” kilisema chanzo hicho.

Stori: MARCO MZUMBE, Dar es Salaam

Leave A Reply