The House of Favourite Newspapers

Bilioni 131/- zatengwa elimu bure

1

jkalRAIS John Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa fedha kwa ajili ya kutimiza ahadi ya kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, zimetengwa Sh bilioni 131 mwezi huu na kupelekwa moja kwa moja katika shule husika.

Amesema Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa, watapatiwa nakala za taarifa za ugawaji wa fedha hizo na kuonya kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayethubutu kuzitumia vibaya.

Rais Magufuli alisema hayo Ikulu Dar es Salaam jana muda mfupi baada ya kupokea ujumbe maalumu kutoka kwa Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe aliyemtumia salamu za pongezi kwa kuchaguliwa kuiongoza Tanzania.

Dk Magufuli aliongeza kuwa fedha hizo ambazo ni pamoja na fedha za maendeleo, fedha za mitihani na fedha vifaa vya ku fundishia zitaanza kutumwa kila mwezi kuanzia mwezi huu.

Katika kipindi cha kampeni, Rais Magufuli aliahidi kutoa elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari kidato cha nne na hivi karibuni kupitia Wizara ya Elimu ilitoa waraka maalumu wa kusisitiza agizo hilo la elimu bure.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amempongeza Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk Philip Mpango kwa kazi nzuri ya ukusanyaji wa mapato inayofanywa na mamlaka hiyo.

“Kwa mara ya kwanza mwezi huu ukusanyaji wa mapato hayo unatarajiwa kuwa zaidi ya shilingi trilioni moja na bilioni mia tatu,” alisema Rais Magufuli katika taarifa hiyo iliyotolewa jana na Ikulu.

Rais Magufuli pamoja na mambo mengine, jana alipokea ujumbe maalumu wa maandishi kutoka kwa Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe uliowasilishwa na Waziri wa Nchi anayeshughu likia Mambo ya Nje ya Japan, Seiji Kihara.

Ujumbe huo umemueleza Rais Magufuli kuwa Japan imeridhishwa na hatua ambazo Serikali ya Tanzania inazichukua katika kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuahidi kuongeza msukumo kwa upande wa Japan katika kuharakisha utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Japan nchini.

Mjumbe huyo juzi alishuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ujenzi wa njia ya umeme yenye urefu wa kilometa 441.5 kutoka Singida – Manyara – Namanga na kuunganisha hadi Kenya, ambapo Japan imetoa mkopo wa Dola za Marekani milioni 96 ili kufanikisha mradi huo.

Akizungumza baada ya kuagana na Mjumbe huyo Maalumu, Rais Magufuli alisema kwa kuwa Tanzania inaelekea kuwa na umeme wa ziada, mradi huo ukikamilika utaiwezesha kuuza umeme nje nchi.

Kuhusu ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme wa gesi wa Kinyerezi II, ambao Japan imetoa mkopo wa Dola za Marekani milioni 292 kwa ajili ya kuutekeleza, Rais Magufuli alisema baada ya kubana matumizi katika bajeti ya serikali, wiki hii Tanzania itakamilisha utoaji wa kiasi cha Dola za Marekani milioni 51.8 ambazo ni sawa na asilimia 15 ya fedha zote zitakazogharimia ujenzi huo.

Aidha, Rais Magufuli alisema taratibu za kuanza ujenzi wa barabara ya juu yaani “Flyover” katika makutano ya barabara eneo la Tazara zimeanza na kwamba jiwe la msingi linatarajiwa kuwekwa mwezi ujao, na kwamba fedha kwa ajili ya ujenzi wa Flyover hiyo ya kwanza nchini zipo na mkandarasi ameshalipwa fedha za awali.

Dk Magufuli pia alizungumzia ujenzi wa barabara nyingine mbili ambazo ni ya Gerezani – Bendera Tatu itakayokuwa na flyover katika eneo la Kamata na Barabara ya Mwenge – Morocco na kwamba Japan imeahidi kutangaza zabuni hizo hivi karibuni

1 Comment
  1. Donnie says

    Haaah, mwanangu namgharamia ‘yunifom’ na kahela ka kununulia ‘bagia’ tu! hahah…

Leave A Reply