NI mshikemshike nguo kuchanika! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia tukio la binti mmoja kumhenyesha vilivyo Mchungaji Daudi Nkuba Mashimo wa Kanisa la Emmaus Bible Church lililopo Mbezi-Luis jijini Dar.
NI STENDI YA MBEZI-MWISHO
Tukio hilo liliibua taharuki ya aina yake mwishoni mwa wili iliyopita na kumpa wakati mgumu Mchungaji Mashimo baada ya kuhenyeshwa na binti huyo katika Stendi ya Mabasi ya Mbezi-Mwisho jijini Dar.
ILIKUWAJE?
Kwa mujibu wa mashuhuda waliozungumza na Risasi Jumamosi, katika tukio hilo, Mchungaji Mashimo, akiwa kwenye huduma zake maeneo hayo ndipo alipoibukiwa na binti huyo aliyekuwa amebeba mafurushi yaliyojaa vitu mbalimbali yakiwemo makopo, chupa, vifuu na vitu vingine vilivyoonekana kuwa vichafu huku akiongea peke yake.
Mashuhuda hao walidai kuwa Mchungaji Mashimo, baada ya kumuona binti huyo katika hali hiyo huku akimfuata kwenye uelekeo wake ndipo alipomkamata na kuanza kumfanyia maombezi kituoni hapo, hali ilizua bonge la mtafaruku wakati binti huyo akikataa maombi hayo.
Mwanahabari wetu, akiwa kwenye majukumu yake ya kila siku alipewa taarifa juu ya tukio hilo na kukimbia ambapo alimkuta Mchungaji Mashimo akiendelea kuhenya katika zoezi hilo.
Hata hivyo, Mchungaji Mashimo kuna wakati alionekana kuzidiwa nguvu na binti huyo kiasi cha kuomba msaada kwa mashuhuda.
KUTOKA MAILI-MOJA, KIBAHA
Baada ya muda, binti huyo alitulia na kuanza kujieleza kwa shida ambapo alisikika akisema anaishi na dada yake maeneo ya Maili-Moja, Kibaha mkoani Pwani.
Binti huyo alipoulizwa alikuwa anaelekea wapi alisema hajui hivyo kusababisha mshangao na minong’ono kuwa huenda alikuwa na tatizo la afya ya akili.
MCHUNGAJI MASHIMO AFUNGUKA
Baada ya vurumai kutulia, Risasi Jumamosi lilimgeukia Mchungaji Mashimo na kumtaka kuelezea tukio hilo ambapo alisema yeye kama mtumishi wa Mungu kazi yake ni kuwahudumia wenye matatizo mbalimbali, hivyo alipomuona binti huyo na mizigo aliyobeba alimuona kuwa hayuko katika ufahamu wa kawaida na hivyo aliamua kumsaidia ingawa alikumbana na changamoto ya aina yake.
“Mimi ni mtumishi wa Mungu ambaye kazi yangu ni kuwakomboa wanaopatwa na mateso na kuelemewa na mizigo.
“Nilipomuona binti huyu nilimuonea huruma na kuanza kumuombea na sasa ameanza kupata ufahamu kwani alikuwa amefungwa na nguvu za shetani.
“Hizi nguo unazomuona nazo siyo alizokuwa nazo, hali yake ilikuwa inatisha kama ungemuona kabla ya hapa alikuwa kwenye hali mbaya sana na ndiyo furaha ya shetani kuwaona watu wa Mungu katika taabu za dunia hii.
AMRUDISHA HALI YA UBINADAMU
“Nimemlipia pesa, kina mama wenzake wamemuogesha na hizi nguo alizovaa nimemnunulia mimi muda si mrefu na kumfanya aonekane hivi anavyoonekana katika hali ya ubinadamu,” alisema Mchungaji Mashimo akiahidi kumsaidia arudi kwao Maili-Moja na kumfuatilia maendeleo yake kiroho.
MCHUNGAJI MASHIMO NI NANI?
Jina la Mchungaji wa Mitume na Manabii, Daudi Mashimo almaarufu Komando Mashimo limekuwa maarufu ghafla baada ya kuhusika katika kumtolea dhamana msanii Rutyfiya Abubakary maarufu kama ‘Amber Ruty’ ambaye anakabiliwa na kesi ya kusambaza picha chafu mtandaoni.
Mchungaji Mashimo amekuwa gumzo mitandaoni na mara kwa mara ameonekana akitangaza kumfanyia maombi Miss Tanzania wa 2006 na mwigizaji bora wa mwaka, Wema Isaac Sepetu kisha kufanya utabiri kuhusu watu na matokeo ya mechi mbalimbali za soka kwa maelezo ya kupewa maono na Mungu.
STORI: Richard Bukos, Risasi Jumamosi
Comments are closed.