The House of Favourite Newspapers

Bob Haisa; Mwana Mpotevu Amerejea!

0

 

EWE dada nipe mgongo nataka kupanda mieee…

Kisha tembea taratibu unipekee kwa mamaaa…

Kama wanipe ndaaa nipe mgongooo nipande taratibuuu…

Ukinifikishaaa utafurahii dadaaa ahaaa…”

 

Kibwagizo hiki kinapatikana kwenye wimbo wa kitambo wa Nipe Mgongo kutoka kwa Haidali Said almaarufu Bob Haisa.

Huyu jamaa ni mwanamuziki mkongwe Bongo, mwenye ladha ya kipekee kwenye miondoko ya mduara. Aliwahi kutisha na nyimbo kibao kama Nipe Mgongo, Nisamehe, Mbeleko, Nithamini Nikiwa Hai na Penzi la Karaha.

Penzi la Karaha ndiyo uliomrudisha kwenye gemu kipindi hiki cha janga la Corona.

 

Baada ya kuwa mwana mpotevu kwa siku nyingi kwenye gemu, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA linakusogeza karibu na Bob Haisa katika mahojiano maalum (exclusive) ambapo anafunguka mengi juu ya kurejea kwake kwenye muziki;

 

IJUMAA WIKIENDA: Watu wamezoa kukusikia ukiimba mduara fulani hivi, lakini ngoma yako mpya inaonekana ni kama sebene, kwa nini umeamua kubadilisha mahadhi?

BOB HAISA: Staili hii mpya ya ngoma yangu inaitwa Sebene Fleva ikiwa namaanisha mchanganyiko wa sebene na Bongo Fleva ikiwa na maana ya kufanya kitu cha tofauti.

 

IJUMAA WIKIENDA: Kwa nini umeamua kurudi kwenye gemu kipindi hiki cha Corona?

BOB HAISA: Kutoa ngoma kwa kipindi hiki cha Corona nimezingatia kwamba walioko ndani au kujiweka karantini wenyewe au kwa mujibu wa sheria, hata waliojihifadhi kama ilivyoelekezwa, nao wanahitaji kufarijiwa, faraja kubwa ni kuwapeleka muziki ili wapate burudani kwa kipindi hiki.

 

IJUMAA WIKIENDA: Umejipangaje kusogeza ngoma yako kwenye jamii kupitia mitandao ya kijamii?

BOB HAISA: Nimejipanga, maana ninayo timu ndogo ya wazalendo wenzangu ambao wameamua kujitolea kuniunga mkono, wako mitandao yote ya kijamii kuhakikisha wadau wangu wanaupata muziki wangu.

 

IJUMAA WIKIENDA: Hivi karibuni kuna mastaa kibao wameachia ngoma zao mpya kati ya hizo ipi imekuvutia?

BOB HAISA: Ngoma ambayo naipenda ni ya Wakenya Femi One na Mejja inaitwa Utawezana.

IJUMAA WIKIENDA: Mkeo aliyekupa kibuti kipindi unahaso, akiamua kurudi utampokea?

 

BOB HAISA: Mke wangu hakunipiga kibuti ila tuliachana kwa kuwa riziki ya mapenzi ilikwisha, siwezi kurudiana naye.

IJUMAA WIKIENDA: Kwenye muziki menejimenti ndiyo kila kitu, nguvu ya menejimenti yako ikoje?

BOB HAISA: Kwa sasa sina menejimenti rasmi, isipokuwa napata sapoti kutoka kwa wadau wanaojitolea kizalendo kwa kuwa nilikuwa nimepotea.

 

IJUMAA WIKIENDA: Nani anayekusapoti kwa sasa?

BOB HAISA: Mtu mmoja ambaye anajitoa katika kusapoti kazi zangu kwa nguvu anaitwa John Dotto Kisute, Mkurugenzi wa White Magic ambao wako Dar katika jengo la Dar Free Market.

IJUMAA WIKIENDA: Unafikiria kufanya kolabo na msanii yeyote Bongo?

 

BOB HAISA: Wasanii ambao tayari nimeshathibitisha kufanya nao kazi ni Marioo, Dullayo na pia wako watu ambao wameonesha nia ya kufanya kazi na mimi.

IJUMAA WIKIENDA: Unazungumziaje sanaa kipindi hiki cha Rais Magufuli na enzi zilizopita?

BOB HAISA: Kipindi cha Magufuli kimekuwa cha tofauti kwa sababu kimetuweka huru.

 

IJUMAA WIKIENDA: Ukipewa nafasi ya kukutana na Rais Magufuli utamwambia nini?

BOB HAISA: Nitampongeza kwa mengi, ikiwemo huruma, uwazi, upendo na kulinda rasilimali.

IJUMAA WIKIENDA: Unazungumziaje janga la Corona?

 

BOB HAISA: Corona ni vita kubwa, kikubwa tufuate maelekezo ya wataalam na tukichanganya asili zetu, tusitegemee mawazo kutoka nje, dawa kubwa ni Mwenyezi Mungu.

IJUMAA WIKIENDA: Je, mipango ya kutoa album ikoje?

BOB HAISA: Mikakati ya album iko vizuri, nimerekodi na ninaendelea kurekodi ngoma kali kama nilivyoahidi, album yangu itakuwa na nyimbo kumi na mbili.

 

IJUMAA WIKIENDA: Unazungumziaje mapokeo ya Wimbo wa Penzi la Karaha ukilinganisha na Inuka ambao ni wimbo wako mpya?

BOB HAISA: Penzi la Karaha mapokeo ni mazuri sana. Inuka ni ngoma ambayo imekuwa kama jiwe la kuduwaa, maana pamoja na kuitanguliza bila video, lakini tayari imekuwa gumzo.

IJUMAA WIKIENDA: Je, mipango ya kuanzisha bendi ikoje?

 

BOB HAISA: Nikianza maonesho nitakuwa nafanya na live band, najiweka sawa ili nianzishe bendi yangu.

IJUMAA WIKIENDA: Mbali na muziki una kipaji kingine?

BOB HAISA: Nimejifuza tiba za asili kiasi kwamba kwa tathmini ya kitaalam, mimi ni tabibu. Pia ni mbunifu wa samani za majumbani.

 

IJUMAA WIKIENDA: Umewahi kuwaza kujiingiza kwenye siasa?

BOB HAISA: Niliwahi kuwaza kugombea nafasi fulani ya kisiasa pale Misungwi (Mwanza), baadaye nikajitoa.

IJUMAA WIKIENDA: Unawaambia nini mashabiki wako?

BOB HAISA: Nimerudi na mambo makubwa, waendelee kufuatilia kazi zangu maana ni mwendo wa burudani tu.

MAKALA: HAPPYNESS MASUNGA

 

 

 

Leave A Reply