The House of Favourite Newspapers

Bob Rudala; Sauti Tamu Iliyopotelea Ughaibuni

0

bob2Bob rudala.

Imelda mtema
“NIMEKUCHAGUA wewe, uwe wanguu…wangu wa maisha, wa kufa na kuzikana, sijali maneno ya watu, wasememayo, yaliyopita si ndwele, tugange yanayokuja…”

Hicho ni kibwagizo cha Wimbo Nimekuchagua Wewe wa mwanamuziki mashuhuri wa Muziki wa Dansi, Esrom Rudala ambaye sauti yake ilivuma vyema alipokuwa na Bendi ya In Africa ambayo ilikuwa ikifanya kazi zake ndani na nje ya nchi kabla hajahamishia makazi yake Kalunde Band.

Kibao chake cha Nimekuchagua Wewe licha ya kutoka miaka ya 2000, mpaka leo wimbo huo unapopigwa popote na kwenye sherehe mbalimbali, hasa za harusi, unaleta msisimko wa ajabu na kuufanya uonekane bado mpya.

Kwa muda mrefu amekuwa hasikiki wala kuachia wimbo mpya, mwanahabari wetu amemtafuta na kufanya naye mahojiano kwa njia ya Mtandao wa WhatsApp:

Yuko wapi kwa sasa?
“Kwa hivi sasa sipo nchini, nipo huku nchini Australia nikiwa katika bendi moja ya Cirque Africa, ambayo ni maalum kwa maonesho makubwa ya sarakasi.
“Bendi hii ni kubwa, inajumuisha wanamuziki 38 toka nchi sita za Afrika ambayo inajumuisha sarakasi, ngoma na muziki.

Kuna wanamuziki wengine kutoka Bongo?
“Ndiyo, kuna wanamuziki ambao nilitoka nao Tanzania kama Martin Kibosho ambaye ni mpiga ngoma maarufu, Salum Kumpeneke aliyetamba na Wimbo wa Dk. Wangu, Kado Bas, Thomas Nhighula ambaye ni mpiga kinanda, Moses Zamangwa anapuliza Saxaphone na Maneno Uvuruge (solo gitaa) na mimi mwenyewe ambaye ndiye muimbaji.

Ameacha utunzi na uimbaji nyimbo za Kiswahili?
“Japokuwa nafanya kazi hii ambayo ni kama ziara ya kuzunguka Australia na New Zealand kwa kipindi cha miaka miwili lakini bado naendelea kutunga nyimbo zangu na kuimba Kiswahili na mpaka sasa tayari nina wimbo mpya ambayo ni mzuri sana, unaitwa Ujio Wako Mpenzi.

Ameoa?
“Bado sijaoa lakini nina watoto na kati yao kuna mmoja amefuata nyayo zangu lakini napenda wasome kwanza kwani ndiyo urithi wao wa baadaye kwa sababu kama kipaji kipo siku zote.

Unafikiri kwa nini Nimekuchagua Wewe ulikubalika?
“Unajua wimbo wowote ambao unaigusa jamii moja kwa moja watu wengi wanaupenda sana, wimbo huo ulikuwa ukizungumzia ndoa, hata mimi leo nikiusikiliza unanipa amani na faraja na bado unapendwa kila kukicha.

Aliachana na Bendi ya In Africa moja kwa moja?
“Hapana, hata sasa ni kama tupo kampuni moja kwa sababu wanamuziki wa In Africa nao wanafanya ziara kama yangu nchini Ujerumani hivyo ni kama bado tupo pamoja hapa tunapiga kazi tu mpaka kielewe maana tupo kama makundi matatu na lingine lipo hapo Tanzania linaitwa Afro Vibe.

Anatarajia kurudi nyumbani?
“Nyumbani ni nyumbani tu, nitarudi pindi nitakapomaliza kazi huku maana bila kuimba nikiwa nyumbani na kusikika basi leo nisingekuwa huku,” alimalizia Rudala.

Leave A Reply