The House of Favourite Newspapers

Bocco, Ame Warejea Taifa Stars, Kazi Ipo Leo

0

LICHA ya timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars)  kuanza vibaya kwenye michuano ya CHAN, lakini mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa shirikisho la soka nchini (TFF), Cliford Ndimbo, amesema malengo ya kikosi hicho ni kuhakikisha inavuka hatua ya makundi na kutinga hatua inayofuata.

 

Taifa Stars itashuka tena dimbani leo Jumamosi Januari 23, 2021, ambapo itamenyana na timu ya taifa ya Namibia katika mchezo utakaochezwa saa 4:00 usiku kwa saa za hapa nyumbani.

 

Kuelekea mchezo huo, Ndimbo aliyeko nchini Cameroon amesema:

 

“Kiukweli nia ni kupata ushindi ama matokeo chanya katika mchezo unaokuja dhidi ya Namibia, na tunafahamu ni mchezo ambao kwetu ni kama fainali na hata mchezo ambao utabakia dhidi ya Guinea nao ni kama fainali kuhakikisha kwamba katika kundi D, basi tunakuwa ni moja ya timu ambazo zinatoka katika kundi letu kuelekea katika hatua ambazo zinafuata, hilo ndilo lengo katika mashindano haya ambayo tupo hapa nchini Cameroon.”

 

Taifa stars ilipoteza mchezo wa kwanza kwa kufungwa mabao 2-0 na timu ya taifa ya Zambia, na sasa kikosi hicho kinachonolewa na kocha Mrundi, Etienne Ndayiragije, kinahitaji kupata matokeo ya ushindi ili kufufua matumaini ya kusonga mbele katika hatua inayofuata.

 

Kuhusu hali ya kikosi, Ndimbo ameweka wazi kuwa wachezaji ambao walikuwa   majeruhi, John Bocco na Ibrahim Ame, wameanza mazoezi na watasubiri ripoti ya mwisho ya madaktari kabla ya mchezo ili kujua nafasi yao kwenye mchezo dhidi ya Namibia.

Leave A Reply