The House of Favourite Newspapers

Bodaboda wajeruhiwa, waandamana Maswa

IMG_20151124_090832Mmoja wa madereva hao akiwa na majeraha mgongoni.

Na faraja mohamed
MADEREVA pikipiki wanaofanya biashara ya kusafirisha abiria maarufu kwa jina la Bodaboda wilayani Maswa mkoani Simiyu, wameandamana hadi kwenye Ofisi za Usalama wa Taifa Wilaya ya Maswa kupinga hatua ya polisi kuwakamata na kuwajeruhi.

Maandamano hayo yaliyofanyika Jumanne iliyopita mjini humo yalisababisha taharuki na baadhi ya shughuli za kijamii kusimama na jeshi la polisi kushindwa kuyadhibiti.
Vijana hao wakiwa na pikipiki zao pamoja na mabango yenye ujumbe tofauti, walifika kwenye ofisi hizo siku hiyo saa 3:20 asubuhi na baadhi ya bango lilisomeka:

SAM_0350

Madereva bodaboda wakiwa kwenye maandamano.

Tumechoka kunyanyaswa na askari wa usalama barabarani Maswa, wametufanya mradi wao wa kupata fedha za kujikimu kimaisha.”

Wamedai kuwa wamekuwa wakipigwa makofi, mateke na virungu katika sehemu mbalimbali za mwili pindi wanapokataa kukubaliana na matakwa ya askari hao wanapowakamata wakiwa kwenye kazi zao.

Hata hivyo, walieleza kuwa kilichowafanya kuandamana siku hiyo ni kile kilichodaiwa kuwa mwenzao alikamatwa na askari hao na kupigwa kisha kuswekwa ndani siku nzima na kutozwa faini ya shilingi 60,000 bila kupewa stakabadhi inayoonesha fedha hizo zimetolewa kihalali.

Kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Mandalu Kwilasa (pichani) akiwa kwenye kituo cha polisi wilaya alisema kuwa alipigwa makofi, mateke na virungu katika sehemu mbalimbali za mwili wake hali iliyosababisha kupata maumivu makali na kuumia.

“Nilipigwa sana, sikutoka nje siku nne kutokana na maumivu mwilini, polisi hapa Maswa wanatunyanyasa sana, mpaka magari ya binafsi wanayatumia kutufukuzia na kutuzuia kwa mbele,” alidai Kwilasa na kuungwa mkono na Jumanne Haji aliyedai kupigwa Jumatatu ya wiki iliyopita bila hatua yoyote kuchukuliwa kwa askari husika.

Waandishi wa habari wawili, Samwel Mwanga wa New Habari (2006) Ltd na Bruno Francis wa Radio Sibuka FM waliokuwa wakifuatilia sakata hilo kwa Kamanda wa Polisi Wilaya ya Maswa, SSP Claud Kanyorota walijikuta wakikamatwa na kusweka mahabusu lakini baadaye waliachiwa kwa dhamana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, ACP Gemin Mushi alikiri kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa waliwakamata waandishi hao kwa ajili ya upelelezi kujua chanzo cha maandamano hayo.
“Ni kweli tumewakamata lakini nimeagiza wahojiwe kisha waachiwe kwa dhamana, upelelezi unafanyika ili ukweli ujulikane,” alisema Mushi.

Comments are closed.