The House of Favourite Newspapers

Bodi Ya Filamu ni Jipu

0

 

MAKALA NA: BONIFACE NGUMIJE | IJUMAA WIOKIENDA

DAR ES SALAAM: Mwaka 2016, Bodi ya Filamu Tanzania iliongezewa majukumu rasmi na Serikali. Tofauti na kipindi cha nyuma ilipokuwa na kazi ya kuzipa madaraja filamu na kukagua stakabadhi, inatakiwa kufanya zaidi ikiwemo kutangaza kazi za filamu.

Mbali na hivyo, ilipaswa kuhakikisha zinaingiza kazi bora sokoni, kuhakikisha tasnia nzima ya filamu inakua, lakini pia kuhakikisha serikali inapata mapato yake kupitia tasnia hiyo cha filamu. Unaweza kujiuliza mdororo kwenye filamu unatoka wapi?

 

Afisa Mawasiliano na Uhusiano wa Bodi ya Filamu Tanzania, Abuu Kimario (kushoto) akizungumza na mwandishi wa Ijumaa Wikienda.

Kwa mujibu wa Abuu Kimario, Afisa Mawasiliano na Uhusiano wa bodi hiyo, akizungumza na Wikenda, alisema moja ya juhudi ambazo ‘mzazi’ huyo wa filamu anafanya, ni pamoja na kuandaa semina kwa wadau wa sekta ya filamu.

Akimaanisha semina kwa waandishi wa miswada, waigizaji na waandaaji wa filamu na namna ya kuandaa filamu bora zenye kupendwa nchini na kutambulika kimataifa. Kufahamu juu ya mikataba yao, lakini pia zikiwa zinautunza utamaduni wetu. Alisema wamekwishafanya semina ya namna hiyo kwa waigizaji wa kike Bongo, waandishi wa scripts (miswada) na wamekwishatembelea baadhi ya mikoa kutoa elimu ya filamu.

Msanii wa Bongo Movie, Vicent Kigosi ‘Ray’

Haya sasa, wakati huohuo wakifanya hicho wanachokiita wao kuikuza tasnia ya filamu, bado filamu nyingi wanazokagua, kuzipitisha na kuingiza sokoni ni mbovu na za viwango vya chini. Ndiyo maana kuna malalamiko chungu nzima kuhusu Bongo Muvi.

Kama hiyo haitoshi, wanadaiwa kupitisha filamu zilizojaa magumashi. Yaani filamu ambazo mhusika anaonekana amevaa nguo nyeusi nje akiingia ndani inaonekana ni ya pinki au jambazi anavua viatu wakati anaingia ndani kufanya tukio na akitoka anavivaa na kukimbia. Si hayo tu, yapo mengine mengi ya kukera.

Niweke wazi, nilichomuelewa Kimario, pengine wanachofanya Bodi ya Filamu Tanzania si kukuza filamu, ni kuziangalia zinafaa kwa watu wa namna gani, wakubwa au watoto na kuzipa madaraja. Labda hivyo, lakini kama ni kukuza.

Wanatakiwa kufanya zaidi ya hivyo wanavyofanya ikiwemo kuzigomea filamu zinazoleta ukakasi kwenye soko na kuwashauri wasanii nini wafanye, tofauti na hivyo nao ni jipu linalohitaji kutumbuliwa! Ukiachana na hayo, Bodi ya Filamu Tanzania juzikati imeshuhudia wasanii wakiandamana Kariakoo jijini Dar wakipinga wizi wa filamu na uingizwaji holela wa filamu za nje.

Baada ya hapo bodi hiyo ikaita waandishi wa habari na kutoa ufafanuzi juu ya kilichofanyika na uamuzi wa serikali kusimamia mapato yake kwa wafanyabiashara wanaoingiza filamu za nje, pamoja na kuweka uwiano wa filamu hizi sokoni ili wasanii wa Bongo pia wanufaike! Binafsi naona bado kuna tatizo ndani ya bodi, lakini pia hawa wasanii walioandamana wanatumika vibaya.

Hivi huo uwiano wa kibiashara ambao Bodi ya Filamu Tanzania inaamini utakuja kwa kupiga pini filamu za nje ni upi? Ina maana bodi hamfahamu kuwa hawa akina Duma na asilimia tisini ya waigizaji wa Bongo hawamiliki filamu sokoni? Hamfamu kuwa filamu zao zinamilikiwa na Wahindi wanaozinunua kazi zao hadi hatimiliki?

Litakuwa ni jambo la kushangaza ikiwa bodi hamfahamu haya yote. Sipingi jitahada za serikali kupata mapato kwa kuwapiga pini wafanyabiashara wa filamu za kigeni, lakini pia ninachokiona ni kuwasafishia njia hawa Wahindi huku wasanii wakizidi kupauka na kuwa maskini! Bodi mna haki ya kusimamia utaratibu na sheria zilizopo chini yenu, lakini kumbukeni mmesaini mikataba ya kimataifa juu yakutunza haki ya filamu za nje.

Msije mkapelekwa na upepo wa wasanii wasiojielewa halafu baadaye ikawa shida maana tasnia yetu ina upungufu mkubwa mno. Tunaona namna kazi za filamu za nje zinavyotumiwa bila vibali kutoka kwa wahusika pamoja na kuuzwa. Sasa wahusika wakija kudai masilahi yao sijui mtasimama upande upi? Wa mdai au mdaiwa!

Ni vyema kuangalia udhaifu uliopo kwenye tasnia na kuunda mikakati ya kuuondoa, lakini si kufanya jambo linaloonekana lina mrengo wa kuwanufaisha watu fulani!

ILIKUPITA HII YA BONGO MUVI KUANDAMANA?

Leave A Reply