Bodi ya Ligi Kuu Yaridhia ombi la Yanga Kutumia Uwanja wa KMC Complex
BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeridhia ombi la klabu ya Yanga kuhusu kuutumia uwanja wa KMC Complex uliopo Kinondoni, Dar es Saalam kwa michezo yake ya nyumbani iliyosalía kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025.
Taarifa ya leo Novemba 25 iliyotolewa na TPLB imebainisha kuwa uamuzi huo umekuja kufuatia ombi la klabu ya Yanga la kuutumia uwanja huo huku Wananchi wakiwa wametekeleza taratibu zote za kuutumia uwanja huo ikiwemo kupata ridhaa na kuingia makubaliano na wamiliki wa uwanja.
Aidha Bodi itatoa taarifa kwa umma kuhusu mabadiliko yoyote ya tarehe ama muda wa kuanza kwa baadhi ya michezo ya nyumbani ya klabu hiyo, yanayoweza kutokana na mabadiliko haya ya uwanja wa nyumbani.
Katika hatua nyingine, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imefanya mabadiliko madogo ya ratiba ya Ligi Kuu ya NBC ambapo mchezo kati ya Azam FC dhidi ya Singida Black Stars sasa utafanyika Novemba 28, 2024 saa 1:00 usiku katika uwanja wa Azam Complex uliopo mkoani Dar es Salaam badala ya Novemba 27, 2024 kama ilivyokuwa awali.
Mchezo kati ya Dodoma Jiji FC dhidi ya Azam FC sasa utafanyika Disemba 1, 2024 saa 3:00 usiku katika uwanja wa Jamhuri uliopo mkoani Dodoma badala ya Disemba 30, 2024 kama ilivyokuwa awali.
Sababu ya mabadiliko hayo ni kuahirishwa kwa mchezo wa Tabora United dhidi ya Singida Black Stars jana Novemba 24, 2024 ambapo kufanyika kwa mchezo huo leo Novemba 25 kumesababisha kukosekana kwa muda wa kikanuni kuelekea michezo tajwa hapo juu.
Pia Bodi ya Ligi Kuu Tanzania imeuondoa mchezo wa Ligi Kuu ya NBC kati ya klabu ya Singida Black Stars dhidi ya Simba Sc ambao ulipangwa kufanyika kwenye uwanja wa CCM Liti Disemba 1, 2024 kutokana na sababu za kiuendeshaji na utapangiwa tarehe mpya hivi karibuni.