Bomoabomoa; kibanzi kwa wananchi, boriti kwa serikali
DHAMBI haina udogo, ukiitenda huwezi kuisafisha kwa wema bali kuiungama. Naam, hata makosa yaliyofanywa na serikali juu ya raia wake waishio mabondeni katika kile kinachoitwa oparesheni bomoabomoa, hayawezi kutakaswa kwa hoja ya nia njema ya kuwaokoa wananchi hao na mafuriko.
Maswali yako mengi; kwa nini bomoabomoa hiyo iwe na nguvu sana mwaka huu na isiwe hivyo miaka 40 iliyopita? Je, kila oparesheni katika nchi hii ni lazima ifanywe kinyama bila kuzingatia utu?
Kwa nini jicho la serikali ni kali kuona kibanzi cha waishio mabondeni lakini linashindwa kuona boriti lililopo kwa maofisa wake waliovitakatisha baadhi ya viwanja vya wananchi hao kwa rushwa; msumeno wa sheria si kukata mbele na nyuma?
Wahenga husema; kwa mwari kukiliwa na kwa kungwi nako kuliwe! Haiwezekani serikali ikawa mbogo kwa wananchi waishio mabondeni ilhali upo ushahidi wa kutosha kuwa wapo wengi kati ya wananchi hao ambao wanavilipia kodi viwanja vyao serikalini.
Leo kufumba na kufumbua wananchi hao wamekuwa haramu; adui namba moja wa serikali wanaopaswa kuvunjiwa nyumba zao na kuachwa nyikani! Potelea mbali wakiangamia kwa magonjwa ya milipuko, kuvamiwa na wanyama au makundi ya wahalifu. Jambo hili linasikitisha!
Pamoja na nia njema iliyofikiwa hivi karibuni na timu ya mawaziri wa serikali ya Rais John Pombe Magufuli ya kusimamisha zoezi hilo la ubomoaji makazi ya watu kiholela kwa lengo la kutazama upya mchakato wake, bado serikali ina jambo la kutubia uovu ilioufanya kwa raia wake.
Maana ni wazi kuwa, tangu zoezi hilo lianze kuna wananchi wameathirika kisaikolojia, wamedhalilishwa kwa kutolewa kwenye nyumba zao kwa nguvu wakati mwingine bila nguo; watoto wameshuhudia ukatili wa kutisha uliofanywa na maofisa wa serikali dhidi ya wazazi wao jambo ambalo kitaalamu limewaumbia moyo wa ukatili, sijui watamlipiza nani na kwa wakati gani?
Kwa dhambi hizi na nyinginezo, serikali haitatakasika kwa kujificha kwenye nia njema ya kuwaokoa wananchi hao na janga la mafuriko; lazima itubu kuwa ilifanya makosa kuendesha zoezi hilo bila kuwepo kwa tathmini inayozingatia sheria, utu na haki za binadamu.
Nashauri; kwa kuwa serikali imeuona ukengeufu wake ni vyema itakapokuwa ikipitia mchakato wa zoezi la bomoabomoa lililofanyika na litakalofanyika baadaye; kwanza ihakikishe kuwa, watendaji wa serikali waliohusika kuwatakatishia wananchi viwanja hivyo kwa kuwapa hati bandia, wanasakwa mahali walipo na kuchukuliwa hatua za kisheria hata kama wamezeeka kiasi cha kutembelea mikongojo.
Pili, kwa wananchi ambao wana ushahidi wa kutosha kuwa wamekuwa wakilipa kodi za viwanja vyao serikalini, warudishiwe fedha zao kwa sababu makusanyo hayo yalikuwa ni sawa na wizi.
Tatu; kwa wananchi wenye hati za makazi na kwa bahati mbaya nyumba zao zimevunjwa, serikali iwajibike kwa kuwalipa fidia zinazoambatana na madhara mengine yaliyotokana na zoezi la bomoabomoa lililofanywa.
Maana ziko taarifa kuwa, kuna baadhi ya wananchi wamepoteza maisha katika oparesheni hiyo huku wengine wakitajwa kupata mshtuko uliowasababishia ulemavu wa mwili.
Nne; kwa wale ambao maisha yao ya mabondeni yalikuwa ni uvamizi uliotokana na usimamizi hafifu wa sheria za nchi; watu hawa ni vyema kwa uungwana wakatafutiwa maeneo mengine ya kuishi kwa sababu Tanzania haijapata kuwa na uhaba wa ardhi kwa wananchi wake.
Tano; ujengwe mfumo utakaowafanya wananchi kuyaheshimu maeneo yasiyo rasmi sambamba na maofisa wa serikali kuwajibika ipasavyo kuyasimamia maeneo hayo ili kuepukana na hasara zinazowapata wananchi wanaotumia fedha nyingi kujenga katika viwanja visivyor