The House of Favourite Newspapers

Bonanza Hili la Wafanyakazi Lilinoga Sana Aisee!

0
Dar es Salaam 30 Septemba 2024: Zaidi ya wafanyakazi 300 wa Kampuni ya Ulinzi  ya SGA walikuwa na bonanza la aina yake na la kuvutia hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya kutimiza miaka 40 tangu ianze kutoa huduma nchini.
Tukio hilo la kuvutia lilifanyika Hekima Gardens jijini Dar es Salaam na wafanyakazi wa SGA walishiriki katika shughuli mbalimbali zilizoonyesha vipaji vyao mbalimbali na wakati huo huo kuonyesha moyo wao wa kukuza michezo na kujenga ushirikiano.
Shughuli zilihusisha mpira wa miguu, rede, mbio za magunia, limao kwenye kijiko, mashindano ya kucheza, kuvuta kamba na kulikuwa na maonyesho mazuri ya moja kwa moja yaliyowafanya waalikwa kuimba na kucheza.
Miongoni mwa waliohudhuria ni daktari bingwa wa magonjwa ya akili na msemaji wa kutia motisha, Dk Kweka, ambaye aliwapa somo wafanyakazi hao katika kikao kilichovuta nadhari alipokuwa akiwashirikisha uzoefu wa aina ya mitindo ya maisha yanayoathiri watu wengi mahali pa kazi.
Kilele cha siku hiyo kilikuwa wakati Mkurugenzi Mkuu wa SGA, Bw Eric Sambu, alipoongoza wafanyakazi kukata keki maalumu.
Bw Sambu aliwashukuru wafanyakazi kwa kujitolea kwao na kuifanya kampuni kupata mafanikio makubwa ndani ya miaka 40 ya kufanya kazi nchini Tanzania. “Mafanikio tuliyopata wakati huu wote yamechangiwa na kujitolea kwenu kwa kampuni,” alisema.
Aidha, alibainisha kwamba bonanza hilo lilikuwa njia ya kuwaleta wafanyakazi pamoja na kusherehekea mafanikio ya kampuni wakati wa kuadhimisha miaka 40. “Hili litakuwa tukio la kila mwaka na kuanzia mwaka ujao tutapanga kulifanya kwa siku mbili ili kuwa la kusisimua na la ushindani zaidi,” alisema, huku wafanyakazi wakishangilia na kupiga makofi.
Mkurugenzi Mtendai wa SGA Tanzania, Bw. Eric Sambu (mwenye kofia na miwani) akiongoza wafanyakazi wa kampuni hiyo katika zoezi la kukata keki wakati wa bonanza la wafanyakazi wa kampuni hiyo lililofanyika jijini Dar es Salaam ilikwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 40 tangu SGA Security ianze kufanya shughuli zake nchini.
Bw Sambu aliwashukuru wateja wao wote na wadau wengine, likiwemo Jeshi la Polisi, ambalo alisema limekuwa likishirikiana vyema na SGA katika utendaji wake kwa miaka yote.
Kwa upande wake, Meneja Mauzo na Masoko, Bi Faustina Shoo, alisema bonanza hilo lilikuwa njia maalumu ya kuadhimisha miaka 40 kutokana na wafanyakazi kujitokeza kwa wingi kwenye maadhimisho hayo.
“Tunajivunia wafanyikazi wetu ambao ndio sababu ya mafanikio haya yote, kwa hiyo tuna kila sababu ya kusherehekea na kufurahia kama wanavyofanya hapa,” aliongeza.
Mmoja wa wafanyakazi hao, Nash Stewart, ambaye amefanya kazi na SGA kwa takribani miaka 30, aliushukuru uongozi kwa kuandaa bonanza hilo, kwani limewafanya wafanyakazi wajisikie ni wa kipekee na wanathaminiwa. “Ni hali hii ya kujisikia vizuri kwani tumeshiriki katika shughuli mbalimbali kama vile michezo, kula, kucheza na mzungumzaji wa kutia motisha alikuwa ni wa pekee,” alisema.
Bw Proches Peter, ambaye ni Meneja Ufundi wa SGA, alisema amefanya kazi na SGA kwa zaidi ya miaka 20 na kuongeza kwamba anajisikia vizuri kuwa sehemu ya tukio hilo la kihistoria, kwani kampuni imetimiza miaka 40. “Najivunia kuwa sehemu ya kumbukumbu hii na siwezi kufikiria kufanya kazi sehemu nyingine kwa sababu kampuni hii imekuwa kama nyumbani kwangu sasa,” alisisitiza.
SGA ilikuwa kampuni ya kwanza kuendesha shughuli binafsi za ulinzi nchini Tanzania kwa takribani miaka 40 iliyopita. Kwa sasa imeajiri zaidi ya Watanzania 5,000 katika mtandao wake katika matawi mbalimbali nchini.
Kampuni pia inatoa huduma za usafirishaji wa bidhaa za thamani, ulinzi, shughuli za dharura na kuweka na kufanya matengenezo ya vifaa ya kietroniki vya ulinzi. Kampuni imejinyakulia vyeti kadhaa vya ISO na imeshinda tuzo nyingi za juu nchini na katika kanda kwa utoaji wa huduma bora.
Leave A Reply