The House of Favourite Newspapers

Bongo movies, twendeni na kasi ya Magufuli!

0

KWENU mastaa wa Bongo Movies. Sina haja ya kuwataja majina maana najua nikifanya hivyo, naweza nikajaza ukurasa huu. Lakini nawasalimu wote katika jina la Bwana!
Poleni na mihangaiko ya kila siku.

Mimi ni mzima wa afya, namshukuru Mungu naendelea na mapambano katika eneo langu kuendana na kasi ya rais wetu, Dk. John Pombe Joseph Magufuli na kauli mbiu yake ya Hapa Kazi Tu.

Nimewakumbuka leo kwa barua maana najua wengi wenu hatujaonana hivi karibuni. Ni vyema pia mkasoma kile ambacho ninacho rohoni na mkakifanyia kazi. Najua mnajua lakini si vibaya nikawakumbusha ili kuweka msisitizo.

Dhumuni la kuwaandikia barua hii ni kutaka kuwaambia kwamba, mnapaswa kujiandaa na ujio wa Dk. Magufuli katika tasnia yenu. Kasi aliyoanza nayo, ni dhahiri kwamba atawafikia muda si mrefu.

Kwa muda mrefu mlikuwa mkilia na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika kazi zenu. Mlikuwa mkisumbuliwa sana na wanyonyaji wa kazi zenu. Wasambazaji wachache walikuwa wakiwapangia bei wanazotaka kununua filamu zenu, tena hati miliki zinakuwa za kwao.

Msanii anaigiza yeye, hati miliki inakuwa ya ‘mdosi’. Anauza anakotaka bila kuwa na mipaka. Wezi wa kudurufu kazi zenu ni tatizo sugu. Mikataba ilikuwa haikidhi matakwa ya msanii kiasi ambacho hakuna aliyekuwa anainjoi maisha ya uigizaji kama walivyo wasanii wa Nigeria, Ghana na kwingineko.

Lakini ninapowaambia mjiandae, namaanisha nyinyi wenyewe pia muamke na muanze kujiandaa na kasi ya maendeleo. Baadhi yenu mlikuwa hamjitambui. Mlikuwa hamna misimamo katika maamuzi yanayohusu kazi zenu.

Ndiyo maana kulikuwa na baadhi yenu walikuwa wanapata kipato chenye nafuu lakini wengine wengi wakiwa na hali mbaya kupindukia. Si muda tena wa kuendeleza majungu, usaliti na vitu kadha wa kadha vinavyofanana na hivyo.

Mnapaswa kuipokea kasi ya Magufuli kwa kuendana na mfumo atakaouweka kusimamia mapato yenu. Mnapaswa kuungana na kupeleka mapendekezo yenu katika ofisi yake. Afanye nini ili muweze kudhibiti wizi wa kazi zenu.

Afanye nini ili muwe mnalipa kodi halali na stahiki huku mkinufaika kwa kipato kizuri. Muwe mnamiliki kazi zenu. Muwe na nyenzo nzuri za kufanyia kazi zenu ili angalau muweze kuzisogelea levo za kimataifa. Amkeni sasa, mnapaswa na nyinyi kuishi kwa kutegemea sanaa.

Muwe matajiri wakubwa kama wasanii wenzenu ambao tunawasoma kila siku kwenye vyombo vya habari ndiyo wenye fedha kuliko hata viongozi wa nchi na wafanyabiashara. Sanaa inalipa kama tu mtaamua kuifanya ‘serious’.

Rais wetu ameonesha mwanga wa kushughulika na mafisadi, rushwa na tunaamini mambo yatakuwa sawa hivyo msimuangushe. Nendeni na kasi yake ili muweze kupiga hatua ya kweli na wakati sekta nyingine zitakapokuwa zinashangilia ushindi wa kasi ya Magufuli na nyinyi pia muweze kufanya hivyo katika eneo lenu.

Ni matumaini yangu Mungu atawaongoza na mtapiga hatua, kila la kheri. Mimi ni ndugu yenu;

………………………….
Erick Evarist

Leave A Reply