The House of Favourite Newspapers

Bongo muvi; Tuzo za Lulu, Rich ziwe somo kwenu!

0

lulu3422 (1)Lulu akiwa amelala na tuzo yake.

KWENU mastaa wa Bongo Muvi. Nawasalimu kwa umoja wenu maana najua siwezi kuwataja majina mmojammoja, maana kwa jinsi mlivyo wengi, nikiwataja nitajaza ukurasa huu.
Vipi mnaendeleaje na hali? Kazi zinakwenda? Poleni kwa majukumu na kwa wale ambao kwa namna moja au nyingine afya haiko sawa Mwenyezi Mungu awafanyie wepesi, mpone haraka na mrudi katika shughuli zenu za kila siku.

Mkitaka kujua hali yangu, mimi sijambo. Namshukuru Mungu kwa kunijalia afya njema.  Niko poa. Naendelea kupambana katika eneo langu kuhakikisha maisha yanasonga mbele.
Madhumuni ya barua hii ni kutaka kuwaeleza kwamba, mnapaswa kufunga mkanda kwelikweli ili muweze kupata maendeleo ya kweli katika tasnia ya filamu Bongo.

Ndugu zangu, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na Single Mtambarike ‘Richie Richie’ walioshinda Tuzo za African Magic Viewers Choice (AVCA) hivi karibuni nchini Nigeria, wawe chachu na mwanga wa nyinyi kuamka upya na kusonga mbele.

3 (2)Richie akipongezwa na Waziri mkuu Majaliwa.

Kama Lulu ameweza kuchukua tuzo hiyo na kuwagaragaza wengine, inamaanisha uwezo tunao. Lakini kinachosikitisha ni kwamba kwa kipindi kirefu kumekuwa na ukimya wa sanaa yetu kuvuka mipaka ya Tanzania.

Kazi mnazozifanya zinaishia nyumbani. Mnashindwa kujulikana katika nchi za jirani au Afrika wakati wao za kwao zinafika kwetu, zinakubalika na watu pengine wanazifuatilia hizo zaidi ya za kwao.
Mwamko unakuwa mdogo. Ni mdogo kwa sababu nyinyi wenyewe wasanii hamfanyi jitihada za makusudi kuhakikisha mnapenya nje ya mipaka ya Tanzania. Hamjitangazi. Hamtumii vyombo vya habari kujitangaza wakati fursa hiyo ipo hususan kupitia magazeti ya Global Publishers.

Mwamko wa kuwapigia kura pale inapotokea msanii mwenzenu ameteuliwa kushiriki tuzo fulani, uwe mkubwa na kweli kila mmoja asiwe na kinyongo. Peaneni sapoti wenyewe kwa wenyewe.
Nakumbuka kipindi cha marehemu Steven Kanumba, alionesha njia katika suala la kujituma. Alionesha juhudi binafsi za kuvuka mipaka ya Tanzania. Alifanya ziara za kujitangaza katika nchi mbalimbali za Afrika.

Alitumia fursa ya kushirikiana na wasanii mbalimbali wa nchi ambazo zimepiga hatua katika tasnia ya filamu kama vile Nigeria na Ghana. Hiyo ilimpa nafasi kubwa ya kuweza kupata soko la kimataifa.

Alijitahidi kufanya kazi zenye ubora. Bahati nzuri tukawa tunaona ushindani hata kwa baadhi ya wasanii waliokuwa wanataka kufanya kama yeye, ile ilikuwa ni dalili njema kama Mungu angemuweka hai mpaka sasa.

Lakini pamoja na kwamba Kanumba ametangulia, bado tunaona jitihada za baadhi ya wasanii ambao mnaendeleza gemu. Kupitia mwanzo mzuri wa Lulu na Richie, tunataka kuona jitihada zaidi.

Ongezeni maarifa. Ongezeni bidii. Toeni kazi zenye ubora wa kuulinganisha na soko la kimataifa. Jitangazeni katika vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii. Nina hakika mtafika mbali kwani vipaji adimu vipo Bongo lakini tunashindwa kufanikiwa kwa sababu ya uvivu, kujiona tumeshafika na kutopenda kujituma.

Mungu awe nanyi na nitawaandikia barua nyingine siku nyingine pale itakapobidi.
Wasalaam;

……………………..
Erick Evarist

Leave A Reply