The House of Favourite Newspapers

Bonta Heshimu Jero, Heshimu Buku, Wana Wanywe Bia

ALIANZA kwa kupondwa mawe kwa sababu ni mti wenye matunda, akaona isiwe kesi, akaamua kuuza kura yake, akaonekana shujaa, lakini alipoliita gemu la Hip Hop, kwamba ni ‘Baby’ wake, akaonekana anafanya matusi, hakupenda kuwaangusha mashabiki akaamua kumsaka mrembo aliyemuita ‘beautiful’, watu wakapiga shangwe hasa alipotokomeza ‘zero’, ndipo alipoamua kuwabariki washikaji zake wakate bia!

 

Unaweza kujiuliza huyu ni nani si ndiyo? Usipate tabu, huyu ni mwanamuziki wa Hip Hop, kwenye wimbo wake uitwao M.A.T.U.S.I, alisema ana undugu na wanaharakati kama Escobar, anatoka Kundi la Weusi, jina linalomtambulisha zaidi kwenye gemu ni Bonta Maarifa.

Bonta, ambaye ni daktari huko Kahama, mkoani Simiyu si jina geni kwa wapenzi wa Muziki Bongo hasa wa Hip Hop.

Hivi karibuni Bonta ameachia wimbo uitwao WWB (Wana Wanywe Bia), wimbo ambao umepokelewa vizuri na kuwa gumzo kila kona kwenye mitandao na mitaani, kutokana na kile alichokiimba.

 

Tofauti na kawaida yake, kukaza kwenye biti ngumu za Hip Hop, Bonta, katika wimbo huu wa WWB, amepenyeza ujumbe kwenye biti f’lan hivi ya ‘trap’, ambayo imefanywa na Q The Don A.K.A Nick OT na video ikitengenezwa na dairekta mkali kutoka Arusha aitwaye Freeman Richard.

Showbiz Xtra, imemtafuta Bonta ili kuweza kuzungumza naye mawili matatu kuhusiana na wimbo huo, huyu hapa msikilize;

Showbiz: Hongera kwa ngoma kali Bonta, hebu waeleze mashabiki idea hasa ya wimbo huu ilitokana na nini?

 

Bonta: Idea ilipatikana hivi; aliwahi kutokea daktari aliyekuwa anategemewa sana kwa upasuaji karibia Kahama nzima, tuliyekuwa tunafanya naye kazi.

Daktari huyu alitumbuliwa kutokana na kuwa na cheti feki cha kidato cha nne. Unajua inauma eeh, mtu tegemezi kama huyo lakini cheti kilimuangusha. Hii ni hali ambayo imewatokea pia wengi, kwa hiyo nilikuwa nafanya kitu fl’an hivi cha kuwatia moyo wote waliyopatwa na mkasa kama huu na mambo mengi yanayoendelea nchini.

 

Showbiz: Wakati huu tunaona umekuja tofauti kidogo na umekaa kwenye trap tofauti na huko nyuma, umekaa kwenye mdundo wa trap, nini hasa kimefanya utoke kiivi?

Bonta: Kama nilivyosema hapo awali, nilikaa na hii idea muda mrefu. Nilikuwa ninatafuta namna ya kufikisha ujumbe kwa kile nilichonacho, lakini si moja kwa moja.

Sasa Q, aliponitumia biti ya namna hiyo nikaona ndiyo sehemu muafaka kufanya kile nilichokuwa ninahitaji kufanya.

Showbiz: Ulitumia muda gani, kutunga mpaka kurekodi?

Bonta: Siku kama tatu hivi.

Showbiz: Kila ulichokiandika kinamaanisha ukweli kwenye maisha halisi?

Bonta: Ndiyo.

 

Showbiz: Umesema kwenye wimbo unakata kila kitu kasaro poda ‘unga’, ni kweli?

Bonta: Hapo nilikuwa ninamaanisha kwenye suala zima la kodi. Mtu anayekunywa bia, analipa kodi kwa sababu ananunua hadharani na analipa bili. Anayenunua sigara hivyohivyo pia, lakini anayenunua unga analipa

 

kodi wapi? Unga ni biashara haramu, kwa hiyo hawa watu hawalipi kodi.

Showbiz: Vipi kuhusu ulivyoimba kutumbua mpaka mimba?

Bonta: Kila mtu anaona kila kitu kinachoendelea nchini. Hii ni Tanzania ya viwanda, kwa hiyo mambo mengine hayana nafasi. Ukifanya unatumbuliwa tu!

Showbiz: Ulimaanisha nini uliposema kwamba laki si pesa imetuponza na watu waheshimu jero na buku?

Bonta: Hali kwa sasa ni ngumu, watu walizoea laki na sasa ni buku, haina budi kuheshimu wakati tulio nao.

 

Showbiz: Kwa muziki unaoufanya, umekwishawahi kuwaza kushirikisha wanamuziki wa nje ili kufikisha ujumbe mbali zaidi?

Bonta: Ndiyo,kama nikipata nafasi. Unajua, sijawahi kutoka nje ya nchi kimuziki toka nimeanza kufanya gemu. Iwe kwa kolabo au ziara ya shoo. Kwa hiyo ikitokea nikapata nafasi hiyo nitafanya.

Showbiz: Hujawahi kutoka nje kimuziki, unafikiri muziki wako pia unatoka nje?

Bonta: Ndiyo unatoka nje. Kuna kipindi niliwahi kwenda Kenya, nilishangaa sana namna watu wanavyonifahamu. Huwezi amini nilipata taarifa mpaka Wimbo wa Nauza Kura Yangu ulikuwa unatumika kwenye kampeni.

 

Showbiz: Faida kwenye muziki wako unaipataje? Kwa mauzo ya nyimbo, shoo au kipi hasa?

Bonta: Sanasana ninalipwa na Mtandao wa Mkito. Lakini ni kiasi kidogo tu. Sifanyi shoo sana, kwa mwaka ninaweza kufanya mara mbili tu au moja.

Showbiz: Watu wangependa kufahamu pia, wewe ni daktari, wakubwa wako wa kazi wanachukuliaje suala la wewe kufanya muziki?

Bonta: Kiukweli wanajivunia. Kwa sababu, ninafanya kazi yangu vizuri na muziki wangu ninaufanya vizuri. Hapa ni taaluma na kipaji, kwa hiyo wanafahamu ninachokifanya na hawana shida na hilo.

Showbiz: Muziki umewahi kukuletea shida kwenye muziki wako?

 

Bonta: Ndiyo. Mwanzoni wakati ninaanza kazi huku Kahama, kuna wakati nikiwa kwenye chumba cha daktari nje foleni ya wagonjwa kwangu ilikuwa ndefu sana. Lakini watu wakiingia chumbani unakuta si wagonjwa. Ni watu wanataka sapoti ya muziki.

Ilifika hatua mpaka nikawa natibu watoto na kina mama kutokana na changamoto hiyo. Lakini kwa sasa haipo tena, kwa sababu nipo kwenye utawala zaidi na sikutani na wagonja sana.”

Showbiz: Una nini cha kumalizia Bonta?

Bonta: Vijana wafanye kile wanachopenda kufanya kwenye maisha. Wasiache shule kwa sababu ya vipaji vyao. Lakini wasiache pia vipaji vyao kwa sababu ya shule. Ni suala la kutenga muda, ninawapenda pia mashabiki zangu sana!

Comments are closed.