The House of Favourite Newspapers

BOSI CHUO KIKUU AJIUA KWA SUMU

MENEJA Rasilimali Watu wa Chuo Kikuu Huria (Open University au OUT), Brown Ngingo anadaiwa kujiua kwa kunywa sumu, nyumbani kwake Mbezi-Jogoo jijini Dar.  Tukio hilo lililokuwa na usiri mkubwa kutoka kwa wanafamilia lilijiri hivi karibuni huku ikidaiwa kuwa, kabla ya kifo hicho, Ngingo alikuwa kwenye mgogoro na mkewe ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja.

CHANZO CHASIMULIA

Chanzo makini kilichokuwa jirani na marehemu kilidai kuwa, Brown aliishi na mkewe kwa takriban miaka 10 kisha wakatengana.

CHAZIDI KUFUNGUKA

Chanzo hicho kilizidi kudai kuwa, baada ya kutengana, mkewe alikwenda mahakamani kufungua kesi ya kudai mali zake ikiwemo nyumba ambayo alikuwa akiishi na mumewe.

“Alipokwenda mahakamani kesi ikaunguruma kwa muda na hatimaye mke akashinda hivyo marehemu akatakiwa kukabidhi nyumba waliyokuwa wakiishi,” kilidai chanzo hicho. Hata hivyo, Ijumaa Wikienda halikuweza kubaini kama ni kweli kulikuwa na ugomvi huo au kulikuwa na jambo lingine tofauti.

SIKU YA TUKIO

Chanzo hicho kilidai kuwa, baada ya mke kushinda kesi, aliichukua kampuni ya udalali kwa ajili ya kwenda kumtoa Ngingo kwenye nyumba hiyo na siku hiyohiyo ndipo alipojiua.

“Siku hiyo ilikuja kampuni ya udalali, ikafika katika nyumba ya marehemu, ikamueleza azma yao, wakaenda kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi- Jogoo kumfahamisha, lakini kabla hawajarudi ndiyo Ngingo alipochukua uamuzi wa kujiua,” kilidai chanzo hicho.

MKEWE ATAJWA

Taarifa mbalimbali zilizokuwa zikizungumzwa msibani hapo zilidai kuwa, chanzo cha marehemu kufikia hatua hiyo ni kitendo cha mkewe huyo kumzidi na kushinda katika kesi hiyo.

“Chanzo cha yote haya ni mkewe, inaonekana kuna kitu ambacho alikifanya kumzidi ujanja mumewe katika nyumba hii jambo ambalo lilimfanya marehemu aone kabisa anakwenda kudhalilika hivyo kuamua kukatisha maisha yake,” alidai mmoja wa majirani, lakini hata hivyo, gazeti hili halikuweza kuthibitisha madai hayo.

AAGWA CHUONI

Ijumaa iliyopita, Ijumaa Wikienda lilifanikiwa kufika katika Viwanja vya Chuo Kikuu Huria (Open), Kinondoni jijini Dar na kukuta ndugu, jamaa na marafiki wakiaga mwili wa marehemu tayari kwa ajili ya mazishi yaliyofanyika katika Makaburi ya Kinondoni, Dar.

MKEWE ADAIWA KUTOFIKA

Ijumaa Wikienda lilipojaribu kudodosa juu ya uwepo wa mkewe katika tukio hilo la kuaga, lilielezwa kuwa hakuweza kufika bila kujulikana sababu. “Mh! Hajafika, lakini hata hivyo sidhani kama anaweza kufika kutokana na mazingira yenyewe,” alisikika mmoja wa waombolezaji.

NDUGU WANASEMAJE?

Ijumaa Wikienda lilijaribu kuzungumza na kaka wa marehemu, lakini hata hivyo, alimtaka mwandishi wetu kuonana na ndugu yao mwingine aliyemtaja kwa jina la Goodluck.

Alipoulizwa Goodluck kuhusiana na chanzo cha kifo cha Ngingo na mazingira yake, hakutaka kuzungumza kwa undani zaidi ya kusema kwa kifupi kuwa marehemu amejiua. “Amejiua,” alijibu kwa kifupi. Ijumaa Wikienda: Tulisikia kwamba alikuwa na ugomvi na mkewe na ndiye aliyesababisha haya yote sijui hilo lina ukweli kiasi gani?

Goodluck: Atakuwaje na ugomvi na mkewe wakati walishaachana? Jitihada za gazeti hili kutaka kujua kwa undani zaidi wa tukio hilo hazikuweza kuzaa matunda kutokana na ndugu wa marehemu kugeuka mbogo na kukataa kabisa kuzungumzia.

MWENYEKITI AONGEA

Baada ya ndugu kukataa kutoa ushirikiano, Ijumaa Wikienda lilipokuwa katika Makaburi ya Kinondoni lilifanikiwa kuzungumza na Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa wa Jogoo, Boniventure Vasolela, mtaa aliokuwa akiishi marehemu ambapo alielezea jinsi tukio lilivyotokea.

“Siku hiyo nilikuwa ofisini kwangu, wakaja madalali wakiwa na amri ya mahakama wakaniambia wanataka nikawakabidhi nyumba ya Ngingo ambayo alijenga na mke wake. “Nikawaambia kwamba siwezi kuwakabidhi hadi nitakapomuona mke wa Ngingo, sasa kumbe wakati ninazungumza na hao madalali, Ngingo kumbe alikuwa ameshafika kule kwenye nyumba yake,” alisema mwenyekiti huyo na kuongeza:

“Sasa tukavutanavutana pale mimi nikaondoka kwenda kufanya majukumu yangu mengine, kabla sijafika mbali ndipo nilipoletewa taarifa za kifo hivyo nikarudi na kukuta tayari Polisi wameshauchukua mwili wa marehemu. Inasemekana alijiua kwa sumu.”

NDUGU WAJA JUU

Wakati mwanahabari wetu wakimalizia mazungumzo na mwenyekiti, waliibuka baadhi ya watu waliosemekana ni ndugu wa marehemu na kumtaka mwandishi aache kuzungumza na mwenyekiti huyo. Watu hao walienda mbali zaidi kwa kutaka kumpiga mawe mwandishi wetu, jambo ambalo lilimfanya mwanahabari wetu aamue kuepusha shari na kuondoka makaburini hapo.

STORI:Mwandishi Wetu, DAR

Comments are closed.