Kartra

Bosi Kaizer Chiefs Awafuata Tonombe, Tuisila Yanga

VIUNGO tegemeo hivi sasa ndani ya Yanga, Wakongomani Mukoko Tonombe na Tuisila Kisinda, wamemshawishi Skauti Mkuu wa Klabu ya Kaizer Chiefs ya nchini Afrika Kusini, Walter Steenbok kwenda kutembelea ofisi za klabu hiyo.

 

Tofauti na skauti huyo, viongozi wengine waliofika kutembelea ofisi hizo mpya zilizopo Mtaa wa Samora, Posta jijini Dar es Salaam ni Siyabulela Loyilane naye kutoka Afria Kusini, Rudolfs kutoka Latvia na Andrew kutoka Uganda waliojulikana kwa jina moja moja.

 

Tonombe na Tuisila ni kati ya wachezaji tegemeo katika kikosi cha Yanga waliojiunga nayo msimu huu wakitokea AS Vita ya Kinshasa, Congo.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassani Bumbuli alisema skauti alishawishika kuja kuitembelea Yanga baada ya kupata taarifa za wachezaji Tonombe na Tuisila kujiunga na klabu hiyo katika msimu huu.

 

Bumbuli alisema kuwa skauti huyo alipewa kazi ya kuwafuatilia viungo hao mwaka jana na mabosi wakubwa wa Kaizer Chiefs kwa kutakiwa kwenda Congo kuwatazama, lakini alipofika akapata taarifa za nyota hao kujiunga na Yanga.

 

Aliongeza kuwa baada ya kupata taarifa hizo haraka alirejea nyumbani kwao Sauzi kwa ajili ya kurudisha majibu ya taarifa za nyota hao, hivyo alipofika nchini katika Kongamano la Wanamichezo lililofanyika juzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akaomba kwenda kuitembelea klabu hiyo ya Yanga ili kujua ukubwa na jinsi wanavyojiendesha.

 

“Juzi tulipokea ugeni mkubwa kutoka kwa viongozi mbalimbali wa soka nchini lakini hasa kwa Skauti Mkuu wa Kaizer Chiefs ambaye ni Steenbok aliyeomba kuja kutembelea ofisi zetu na kikubwa kujionea jinsi klabu inavyojiendesha.

 

“Na kikubwa zaidi walitaka kufahamu tuliwezaje kuwaona na kuwasajili akina Tonombe na Tuisila, hivyo mara baada ya kufika ofisini walikutana na Kaimu Katibu Mkuu Mfikirwa (Haji), Mshauri wa Klabu, Senzo (Mazingisa) na Injinia (Hersi Said).“Katika kikao walishauriana mambo mengi ya kuhusu klabu hizi mbili za Kaizer Chiefs na Yanga.

 

“Skauti huyo alielezea mipango yao waliyonayo Kaizer Chiefs ya kuwasajili Tonombe na Tuisila kabla ya sisi kuwasajili kuja kuichezea Yanga, kiukweli alionekana kusikitika kuwakosa wachezaji hao,” alisema Bumbuli

STORI NA WILBERT MOLANDI


Toa comment