The House of Favourite Newspapers

Bosi Yanga Afunguka Morrison Kutua Klabuni, Simba Yatoa Tamko Zito

0
Bernard Morrison akiwa ndani ya uzi wa Yanga

MAKAMU Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, amesema kuwa kiungo wa Simba, Mghana, Bernard Morrison ni bonge la mchezaji, na wanatamani awepo katika kikosi chao msimu ujao.

 

Kauli hiyo imekuja baada ya tetesi nyingi kuzagaa za kiungo huyo kurejea katika timu yake ya Yanga kwa ajili ya msimu ujao.

 

Tetesi hizo za kurejea Yanga zimekuwa nyingi kutokana na kuwepo katika orodha ya wachezaji ambao mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mwakalebela alisema kuwa hakuna timu ambayo isingependa kummiliki Morrison katika kikosi chake kutokana na kiwango bora alichonacho.

 

Mwakalebela alisema kuwa shida ya kiungo huyo ni nidhamu pekee, lakini ndani ya uwanja yupo vizuri kutokana na kiwango kizuri alichonacho ambacho kinaipa timu matokeo mazuri ya ushindi muda wowote katika mechi.

 

Aliongeza kuwa hatima yake ya kurejea Yanga, ngumu kuiweka wazi kutokana na mkataba wake alionao katika timu yake ya Simba.

 

“Nisingependa kulizungumzia suala la Morrison kurejea Yanga, lakini ni mchezaji mzuri atakayekupa matokeo ya ushindi muda wowote akiwepo uwanjani kutokana na kiwango bora.

 

“Ana nafasi ya kucheza katika kikosi chetu kama akirejea tena Yanga, kiukweli Morrison ni mchezaji ambaye kila timu ingetamani kuwa naye.

 

“Shida yake kubwa ni nidhamu pekee, hivyo tusubirie mwishoni mwa msimu kila kitu kitajulikana kipindi ambacho mkataba wake utakuwa umemalizika ndani ya Simba,” alisema Mwakalebela.

 

Yanga iliingia katika mgogoro mzito na kiungo huyo hadi kufikia hatua ya kumpeleka katika Mahakama ya Usuluhishi ya Masuala ya Kimichezo (Cas) ambako Morrison alishinda kesi na kuruhusiwa kuichezea Simba.

 

Timu hiyo ilifikia hatua ya kwenda Cas wa kile kilichoelezwa kusaini Simba akiwa amebakisha mkataba wa mwaka mmoja huku yeye akidai alisaini mkataba wa miezi sita siyo miaka miwili kama Yanga walivyodai.

 

Kwa upande wa Simba, wameweka wazi kuwa hawahofii kumpoteza mchezaji huyo kwa Yanga na wako tayari kumruhusu mchezaji yeyote atakayehitaji kuondoka.

 

Morrison alijiunga na Simba kutokea Yanga Agosti 8, mwaka 2020 katika usajili ambao ulizua mjadala mkubwa.

Morrison alijiunga na Simba kutokea Yanga Agosti 8, mwaka 2020

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Kuhusu Yanga kumhitaji Morrison hilo sio jambo jipya kwetu, tunalijua na hatuhofii, kama viongozi tunafurahi kuona mchezaji wetu anahusishwa nao kwa kuwa hii inatuhakikishia kuwa ni mchezaji mzuri na ndiyo maana wanatamani kuwa naye.

 

“Morrison siyo mchezaji pekee ambaye anazivutia timu nyingine, kama ilivyokuwa kwa Clatous Chama na Luis Miquissone msimu uliopita, mpaka sasa mezani tuna ofa za timu nyingi kubwa ambazo zinawahitaji wachezaji wetu akiwemo Pape Sakho na tunaweza kumruhusu mchezaji yeyote kuondoka.”

Leave A Reply