Bosi Yanga Alichambua Bao la Ntibazonkiza

BAADA ya mshambuliaji mpya wa Yanga, Said Ntibazonkiza ‘Saido’ kufunga bao lake la kwanza katika mchezo wake wa kwanza wa ligi kuu akiwa na Yanga, bao hilo limempa kigugumizi bosi wa Yanga ambaye alishindwa kulielezea.

 

Ntibazonkiza ambaye alisajiliwa na Yanga kupitia dirisha dogo la usajili, amekuwa na kiwango kizuri tangu ajiunge na timu hiyo kwani tayari ameshaifungia timu hiyo mabao matatu katika michezo miwili aliyocheza, ukiwemo mchezo mmoja wa kirafiki.

 

Mshambuliaji huyo alifanikiwa kufunga mabao mawili katika mchezo dhidi ya Singida ambao ulikuwa ni mchezo wa kirafiki, kisha akafunga bao moja na kutoa pasi ya bao moja katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM ambaye pia ni kiongozi wa usajili ndani ya Yanga, Eng. Hersi Said, alisema kuwa hakuelewa mchezaji huyo alifungaje lile bao kwani hakutegemea kuona akifunga kutokana na hali ya mchezo ilivyokuwa kwa wakati ule.“

 

Ni ngumu kuamini kuwa alifunga lile bao, nilipigwa na butwaa maana wakati anafunga lile bao, timu ilikuwa katika presha ya kuhakikisha inapata bao, hivyo kiufupi timu ilikuwa katika wakati ambao sikutegemea kama yeye angefunga bao kwa wakati ule.“

 

Alifunga vizuri na sisi kama viongozi tunajivunia kuwa na wachezaji ambao wanatuonyesha kuwa ni wachezaji wa aina gani, hivyo tukiwa kama viongozi tunawaomba wapenzi na mashabiki wa Yanga wazidi kutuunga mkono ili tupate kile ambacho kipo ndani ya malengo yetu msimu huu,” alisema bosi huyo

STORI: MARCO MZUMBE, Dar es Salaam |  CHAMPIONI

Toa comment