The House of Favourite Newspapers

Bosi Yanga Ataja Sababu Tatu Kuwapeleka Waarab Mwanza

MAKAMU Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, ametaja sababu tatu za kuupeleka mchezo wao wa hatua ya mtoano wa Kombe la Shirikisho Afrika mkoani Mwanza.

 

Yanga inatarajiwa kuvaana na Pyramids FC ya nchini Misri Oktoba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mkoani humo.

 

Timu hiyo tayari imetangaza rasmi kuupeleka mchezo huo huko Mwanza mara baada ya droo ya Caf kuchezeshwa na kuangukia kwa Pyramids.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mwakalebela alisema kuwa kabla ya kuupeleka mchezo huo Mwanza, kwanza walijiridhisha kukidhi vigezo vya kutumika Uwanja wa CCM Kirumba.

 

Mwakalebela Alizitaja sababu hizo tatu ni “Moja, ni kukwepa presha ya mashabiki ambayo imekuwa ikijitokeza kila wanapocheza mechi zao za ligi ya michuano hiyo ya kimataifa, hivyo kama uongozi tunaamini vijana wetu watacheza bila ya presha Uwanja wa CCM Kirumba.

 

“Pili, wachezaji kuuzoea uwanja huo ambao kabla ya kucheza na Pyramids watacheza mchezo wao wa ligi dhidi ya Alliance FC, hivyo wanaamini wachezaji wao watakuwa wameuzoea kwani tumepanga kuendelea na maandalizi ya mchezo dhidi ya Waarab mkoani humo tukiutumia Uwanja wa CCM Kirumba.

 

“Tatu, muhimu zaidi tunawapa nafasi wakazi wa Jiji la Mwanza na mikoa ya jirani kushuhudia mchezo wa kimataifa baada ya kukosa burudani hiyo kwa miaka kadhaa,” alisema Mwakalebela na kuongeza:

 

“Uongozi umepanga kwenda Mwanza mapema kwa ajili ya kuandaa mazingira mazuri ya kambi ikiwajumuisha baadhi ya viongozi wa Kamati ya Utendaji ambao kwa pamoja ulipitisha kuupeleka mchezo huo Mwanza.”

 

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

 

 

 

Comments are closed.