Boss Martha Aibua ‘Vilio’ Upya
ZIKIWA zimepita takribani wiki tatu tangu Tasnia ya Uigizaji (Vichekesho) Bongo kupata pigo kwa kuondokewa na Martha Shilole ‘Boss Martha’, muigizaji huyo ameibua ‘vilio’ upya ukumbini.
Juzikati kulikuwa na onesho ambalo marehemu alikuwa akishiriki pamoja na wasanii wengine lililopewa jina la Cheka Tu, ambapo lilifanyika kwa mara ya kwanza tangu muigizaji huyo kufariki dunia.
Wakizungumza kwa huzuni, mmoja wa waigizaji hao, MC Kisoli alisema kuwa kuondoka kwa Boss Martha kumekuwa pengo kubwa kwao, kwani kwa mara ya kwanza wamefanya onesho lao bila ya kuwa na mwanamke na ndiyo maana huzuni imetawala.
“Hatukuwa tumezoea hali hii, Boss Martha alikuwa ni zaidi ya mwanamke kwani ndiye aliyekuwa mwanamke pekee kwenye onesho hili aliyeweza kuwafunika wanaume wengi, inatuuma sana,” alisema MC Kisoli. Muandaaji wa onesho hilo ambaye pia ni mchekeshaji maarufu, Coy Mzungu naye alisema;
“Kwenye maisha kuna vitu vingi sana vinatokea, hivyo basi naomba watu wote tuishi kwa upendo na amani, na hiki ni kidogo tulichoanza nacho kwa ajili ya mwenzetu aliyetangulia mbele za haki. Tutaikumbuka daima kazi yake na tunaendelea kuithamini, na hiki tunachokifanya leo ni kwa ajili yake japo inauma sana bila ya uwepo wake.”
STORI: AMMAR MASIMBA, DAR
Comments are closed.