Ripoti mpya ya Benki Kuu ya Tanzania imethibitisha kuwa sekta ya utalii (travel and tourism), pamoja na kumaliza mwaka wa kalenda wa 2024 ikiongoza katika sekta zote nchini Tanzania kwa kuingiza fedha za kigeni, imeianza tena mwaka 2025 kwa kukua ikisimama kileleni kwa kufikia rekodi mpya ya Dola Bilioni 3.927
Ripoti hiyo mpya ya BOT ya takwimu za Januari 2025 inaonesha mchango wa utalii ni sawa na asilimia 56.8 ya mauzo yote ya nje ya huduma na kiasilimia ni sawa na asilimia 24.1 ya mapato yote ya fedha za kigeni kwa mwaka huo zilizotokana na mauzo ya bidhaa na huduma mbalimbali vikichanganywa kwa pamoja huku kwa mbali ikifuatiwa na madini (Dola Bilioni 3.5) na Uchukuzi (Dola Bilioni 2.4).
Alipoulizwa mafanikio haya yametokana na nini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi anasema: “Msingi mkubwa ni ule uliowekwa mwaka 2022 na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kujitangaza kimkakati kupitia Filamu ya “Tanzania: The Royal Tour.” kwani katika masoko yote ya asili filamu hiyo iliweza kutusaidia kuongeza idadi ya watalii wa nje na ndani.
“Pili mwaka 2024 tena Mhe. Rais alitusaidia kushiriki filamu maalum na ya kimkakati ya kuitangaza nchi yetu nchini China ambalo ni soko kubwa kila nchi duniani inalikimbilia. Filamu ya “Amazing Tanzania” nayo ikafanya vyema sana maana ilizinduliwa Beijing na hadi Disemba ilileta watalii kutoka nchi hiyo pekee zaidi ya 20,000.”
Anaongeza: “Pia tuliongeza mbinu ya kutangaza utalii wetu kwa kushirikiana na sekta binafsi kupitia vitu viwili: Mosi tunaita “Roadshows” kwa kwenda kukutana na wafanyabiashara katika sekta ya utalii wa nchi nyingine ana kwa ana. Tulikwenda China, India, Ujerumani, Uingereza, Poland na mkakati huu unaendelea.
“Pili tumeimarisha sana mkakati tunaita “Fam Trips” kuwaleta nchini mawakala, wanahabari na watu mashuhuri kuja kuiona na kuitangaza nchi yetu. Mfano alikuja hapa nyota wa PSG Ashraf Hakimi post zake zikasomwa na mamilioni ya watu, walikuja hapa mastaa wa kike “madiva” kutoka China wakaandaa kipindi cha Divas Hit the Road kikaangaliwa na watu Bilioni 1.2 duniani. Mwaka huu 2025 hatupaswi kushuka viwango vyetu na hapa nikugusie tu hivi karibu kuna mastaa wakubwa akiwemo mmiliki wa klabu mashuhuri dunia watatua Tanzania. Kazi inaendelea.”