The House of Favourite Newspapers

BREAKING: Kodi ya Nyumba Yamkera JPM, Atoa Agizo TRA- Video

Rais Dkt. John Magufuli amesema japo kuwa uchumi wa nchi unakwenda vizuri, mfumuko wa bei pia umepungua, lakini Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikisuasua katika majukumu yake ya ukusanyaji kodi hivyo serikali kupata mapato kidogo ikilinganishwa na nchi zenye wananchi wachache.

 

Magufuli amesema hayo leo wakati akizungumza na TRA na Wakuu wa Mikoa nchi nzima katika ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam na kutolea mfano kwamba Msumbiji ina raia milioni 27 na walipa kodi ni milioni 3.3, lakini Tanzania ina raia 55 lakini walipa kodi ni milioni 2.2 pekee na kwamba uwiano wa kodi kwa GDP ni asiliamia 12.8.

 

Rais Magufuli ameiagiza TRA na Wizara ya Fedha kutoza kodi ya nyumba ya TZS 10,000 kwa nyumba za kawaida, TZS 20,000 nyumba za ghorofa zilizopo wilayani na vijijini na Sh 50,000 kwa nyumba kubwa. Tozo hizo zizingatie hati ya kiwanja na sio idadi ya nyumba kwenye kiwanja.

 

“Katika makadirio ya kodi ya nyumba, wapo wanaokadiriwa hadi Sh. Milioni 2 au Sh. Milioni 3. Nyinyi wakuu wa Mikoa ni mashahidi, mtu amejenga nyumba kwa gharama halafu mnatoza kodi hizo, halafu hata bomba la maji hamjaleta.

 

“Watanzania tuko Milioni 55 lakini idadi ya nyumba zinazolipiwa kodi ziwe Milioni 1.9. Natoa wito kwa TRA na mamlaka nyingine za mapato hakikisheni mnatengeneza mifumo rahisi kwa wawekezaji na mpunguze vikwazo.

 

“TRA tumeshindwa hata kurasimisha Sekta ambayo si rasmi ambayo ni asilimia 70, tunakusanya kwenye Sekta rasmi ambayo ni asilimia 30 pekee, tunashindwa kukusanya mapato kwenye Sekta isiyo rasmi, niseme ukweli hatufanyi vizuri kabisa.

 

“Yapo matatizo katika TRA yenyewe, kwenye mgawanyo wa watendaji katika maeneo mbalimbali. Kuna baadhi ya wafanyakazi wanapigwa vita, wanaondolewa na kuwekwa wengine kwa upendeleo. Lipo tatizo la kubambikizia watu kodi kupitia mfumo wa kukadiria. Mtu ana biashara ndogo anakadiriwa kodi kubwa, mwisho wake anafunga biashara, sasa hapo TRA mmepata faida au hasara? Wengine wanafunga biashara na kwenda kufungua upya maeneo mengine.

 

“Mazingira ya kufanyia biashara nchini bado ni tatizo. Usafirishaji, utitiri wa taasisi za usimamizi na tozo, ucheleweshaji bandarini, tatizo la umeme, kutumia muda mrefu kupata vibali vya biashara. Hatufanyi vizuri katika kuvutia wawekezaji.

 

“Askari anaweza kujisikia tu kusimamisha gari hata kwa zaidi ya saa 6 kisha ndiyo akaliachia bila kujali kuwa hao ni wafanya biashara na wanajisikia vibaya, mara nyingi hili linafanywa na jeshi la polisi. Nawataka TPA, TRA, polisi na Idara ya uhamiaji mjirekebishe, vipo vitendo vingi vya kukwamisha wawekezaji naomba mlifanyie kazi,” amesema Rais Magufuli.

 

VIDEO: FUATILIA TUKIO HILO HAPA

Comments are closed.