The House of Favourite Newspapers

Lipumba: Maalim Seif Ataiongezea ACT-Wazalendo ‘Damu Yenye Virusi’ – VIDEO

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Haruna, amesema aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Seifa Sharif Hamad, amekwenda kukiongezea ‘damu chafu  yenye virusi’ chama cha ACT-Wazalendo ili kife kabisa.

 

Lipumba amesema hayo leo Jumanne, Machi 19, 2019 wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, siku moja tangu ashinde kesi yake kutokana na mgogoro uliokuwepo kwenye chama hicho baina yake na upande wa Maalim Seif ambapo jana mahakama ilitoa uamuzi na kumtambua kuwa ndiye mwenyekiti halali wa CUF.

 

Amesema kuwa Mkutano Mkuu wa CUF ulikuwa umeshamfukuza Seif kwa madai ya kukihujumu chama hicho ikiwemo kuwakataza wanachama wake kupeleka mashtaka mahakamani kufuatia mgogoro wa uchaguzi wa mwaka 2015.

 

“Mtu amezuia kesi za wawakilishi wasiende mahakamani matokeo yake hatuna viti vya wawakilishi, badala yake amewafungulia kesi 39 wanachama wenzake, kwa mantiki hiyo mtu huyu hakuwa na nia njema na chama chetu, alifanya haya kukidhoofisha chama. Hivyo mkutano mkuu wa CUF uliamua kumfukuza uanachama Maalim Seif.

 

“Kama ameangukia ACT- Wazalendo acha aipeleke damu yake chafu ACT, na kama ACT iko mahututi, ikaongezewa na damu chafu, yenye virusi, basi wanakwenda kuimaliza kabisa ACT ife, isiinuke na kuinuka,” amesema Prof. Lipumba.

 

Aidha, Lipumba amesema wengine waliotimuliwa ni Ismail Jusa, Salim Abdalla Biman, Joran Bashange, Issa Khery, Mbalala Maharagande na wengine huku akidai kuwa mgogoro huo umekijeruhi sana chama cha CUF.

 

Lipumba amesema katika kudai haki wameshiriki kikamilifu hadi kufikia kupigwa mabomu Januari 27, mwaka 2001 huku baadhi ya wananchi wakipoteza maisha na wengine kujeruhiwa ambapo Lipumba aliwekwa ndani. Kiongozi huyo amedai kwamba wakati wanapigwa mabomu, Seif alikuwa London.

 

“Wakati tunadai haki na kupigwa mabomu huku nikiwekwa jela na wananchi wakiumizwa, Maalim Seif alikuwa Ulaya, anasema tutadai haki tukiwa huku Ulaya na sisi tukamwambia tutadai haki tukiwa hapahapa. Watu walikimbilia msituni na wengine kwenye mashimo. Seif Sharif asitufarakanishe, leo anawaambia wabunge wamfuate huko ili akawatose. Anaonyesha ubabe kwa sababu hataki kufanya kazi na Lipumba.

“Polisi walinipiga saa yangu ikatoka mkononi kabla haijaanguka wakaidaka mpaka leo sijaiona. Kamanda Sirro angalia-angalia huko kwa vijana wako huenda ukaipata saa yangu unirejeshee,” amesema Lipumba huku akiwataka Wazanzibar kuungana na kumpuuza Maalim Seif.

 

MSIKIE LIPUMBA AKIFUNGUKA HAPA

Comments are closed.