WATU watano wamefariki baada ya lori la kampuni ya Dangote lililokuwa limebeba malighafi ya kutengenezea saruji likielekea Mtwara kugongana na gari dogo na kupinduka kisha kuwaka moto wilayani Rufiji.
Moto huo ulitokana na gari hilo kugonga nguzo ya umeme ambapo ilipoanguka, waya wenye moto ukanasa kwenye bodi ya gari hiyo na kuua watu wanne papohapo, na mmoja aliyekuwa kwenye gari dogo akafariki wakati akipatiwa matibabu, wilayani humo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Onesmo Lyanga, athibitisha tukio hilo wakati akizungumza na kituo cha televisheni cha ITV ambapo ameeleza kuwa gari ndogo Toyota Premio ilikuwa ikitokea kwenye makazi ya nyumba za walimu wa Sekondari ya Kibiti eneo la Kinyanya ilipoingia katika barabara kuu inayotoka Dar es Salaam kwenda Mtwara huku gari la Dangote lilikuwa linatokea Dar kwenda Mtwara, ndipo dereva wa gari ndogo aliingia barabarani bila kuzingatia sheria na ndipo ikagongana na gari kubwa la Dangote.
“Kwa bahati mbaya gari la Dangote lilipoteza muelekeo, likaelekea kulia zaidi mwa barabara na kutoka nje na kwenda kugonga nguzo ya umeme, wakati hiyo nguzo ya umeme inadondoka waya wa umeme ukanasa kwenye bodi ya gari na wote waliokuwepo kwenye gari hiyo ya Dangote waliteketea kwa shoti hiyo,” alisema Lyanga.
Amesema dereva na abiria wake watatu waliokuwemo kwenye gari la Dangote waliteketea kwa moto baada ya shoti hiyo ya umeme ambapo mpaka sasa hawajawatambua, lakini abiria wa gari ndogo yeye alikatika vidole vya mguu na akakimbizwa hospitali ya misheni ya Chubwi lakini alifariki, wakati dereva wa gari hilo anapatiwa matibabu hospitali ya Chubwi.
Ameongeza kwamba miili ya watu wanne waliokuwa kwenye gari ya Dangote imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga, ambapo pia amewakumbusha madereva kuhakikisha wanazingatia sheria ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.
Comments are closed.