BREAKING: MBOWE ASEMA KUNA UGONJWA WA ‘BURUDANI’ GEREZANI – VIDEO

MWENYEKITI  wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe,  amesema amekutana na mambo mengi ya kuumiza alipokuwa mahabusu katika gereza la Segerea jijini Dar es Salaam, tangu Novemba 2018.

 

Akizungumza na wanahabari leo tarehe 15 Machi 2019 jijini Dar es Salaam, Mbowe ametaja changamoto zinazowakabili wafungwa katika gereza la Segerea huku akikazia kuhusu tatizo la watu wanaobambikiwa kesi na wanaofungwa bila hatia.

 

“Kuna ugonjwa uliopo magereza kwa lugha ya huko unaitwa ‘Burudani’ ambao ni ugonjwa wa ngozi na unaambukiza, chanzo chake ni kunguni na chawa,” alisema akifafanua kwamba ugonjwa huo unatokana na uchafu unaosababishwa na kutooga kwa muda mrefu na kwa kulala eneo moja na walioamukizwa. 

 

”Segerea kuna mahabusu kati ya 2,300 mpaka 2,450 lakini uwezo wa gereza hilo ni mahabusu 750, watu wanalala kitu kianaitwa ‘mchongoma’ yaani mnalala kwa ubavu mmoja kwa masaa matatu kisha mnageuka,” amesema Mbowe.

 

Mbowe ameshauri vyombo vya kutoa haki viweke mikakati ya namna ya kupunguza mahabusu, akifafanua kwamba vyombo hivyo kama vitapitia vizuri makosa ya mahabusu hao,v itagundua kuwa nusu ya wafungwa walioko magerezani hawakustahili kuwepo huko.

 

”Sisi hatuna tatizo na mifumo yetu ya utoaji haki kwa maana ya mahakama lakini mahabusu wanavyoishi kule magerezani ni kama tayari wote wamehukumiwa na sio watuhumiwa,” amesema na kuongeza:

 

 ”Mimi niombe vyombo vyetu vya kulinda na kutoa haki kwa watu vitafakari namna ya kupunguza hawa mahabusu na kama wataamua kupitia vizuri makosa ya watu, watagundua nusu ya mahabusu wanaojaza magereza zetu ni watu ambao hawakustahili kuwepo kule.”

 

Aidha, Mbowe amesema kuwa askari magereza wanakabiliwa na ukosefu wa sare ambapo wengi wao wanajinunulia.

”Askari magereza hawapewi sare bali wanajinunulia kwa hiyo ukikuta mjanjamjanja anavaa vizuri ila ukikutana na aliyechoka, kachoka kwelikweli.  Niombe tu wawezeshwe, kazi wanayoifanya kukaa na mahabusu sio ndogo kama tunavyodhani,” amesema Mbowe.

 

Toa comment