The House of Favourite Newspapers

Breaking: Mchungaji wa Wake 3 Ahukumiwa Jela na Wake Zake – Video

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imemhukumu mchungaji wa Kanisa la The Early Church of Lord Yeshwah, David Chirhuza (33) raia wa Congo, kulipa faini ya Tsh milioni mbili au kutumikia kifungo jela miaka miwili kwa makossa mawili ya kuishi nchini bila kibali na kuendesha kazi za kanisa bila kibali.

 

Mchungaji Chirhuza mwenye wake watatu amehukumiwa leo Jumanne, Septemba 10, 2019, mahakamani hapo huku wake zake wawili Ester Sebuyange (27), Kendewa Ruth (22) na mdogo wa mchungaji huyo, Samwely Samy wakihukumiwa kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Tsh milioni moja kila mmoja.

 

Awali kabla ya kukiri makosa yao, watuhumiwa hao walikumbushwa makosa yao yanayowakabili na kwa pamoja walikiri na mahakama kupokea hati ya mashtaka kama kielelezo cha awali.

 

Baada ya kukiri makosa yao mahakama hiyo iliwatia hatiani kwa kosa la kwanza la kuishi nchini bila kibali na kosa la pili la kufanya shughuli za kikanisa bila kibali ambapo wote kwa pamoja wameomba mahakama iwapunguzie adhabu.

Mchunguji Chirhuza ameieleza mahakama kuwa si lengo lake kufanya shughuli hizo za kikanisa kwa kujinufaisha kibiashara bali alikuwa akitoa huduma za kimungu kwa wananchi. Mshitakiwa wa pili ambaye ni mke wake, ameiomba mahakama pia kumpunguzia adhabu kwani anasumbuliwa na tatizo la sikio wakati mtuhumiwa watatu akisema anaomba asamehewe.

 

Awali, wakili wa Serikali kutoka Idara ya Uhamiaji, Godfrey Nwijo ameiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa watuhumia hao ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaokabiliwa na mashtaka kama hayo. Washtakiwa walipandishwa kizimbani mapema leo mbele ya Hakimu mkazi Agustina Mmbando wakitokea mahabusu ya Segerea.

 

Akitoa hukumu yake Mmbando amesema watuhumiwa wote kwa pamoja watatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela ama kulipa faini ya Tsh milioni moja, kwa kosa la pili linalomhusu mchungaji kufanya shughuli za kikanisa atalipa faini milioni moja au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela. Hakimu amesema kama watakidhi vigezo hivyo watatakiwa kurudi nchini kwao.

NA DENIS MTIMA | GPL

Comments are closed.