BREAKING: NDUGAI AMSIMAMISHA UBUNGE MASELE KWA UTOVU WA NIDHAMU – VIDEO

SPIKA Job Ndugai ametangaza kusitisha uwakilishi wa Mbunge Stephen Masele kwenye Bunge la Afrika (PAP) ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Bunge hilo kwa tuhuma za utovu wa nidhamu mpaka atakapohojiwa na Kamati ya Maadili ya Bunge.

 

Ndugai ametangaza uamuzi huo leo Alhamisi, Mei 16, 2019 wakati akizungumza bungeni jijini Dodoma.

“Tunao wabunge wanaotuwakilisha kwenye mabunge mbalimbali ya Afrika ikiwemo SADC, Pan African Parliament (PAP), African Caribbean Pacific, Bunge la Afrika Mashariki na Bunge la Maziwa Makuu, wamekuwa wakifanya vizuri katika kutuwakilisha.

 

“Lakini katika Bunge la Afrika (PAP) kumetokea matatizo makubwa hasa kwa Mheshimiwa Stephen Masele ambayo nisingependa kuyafafanua kwa sababu muda hautoshi, tumelazimika kumtafuta na kumrudisha nyumbani kuanzia Jumatatu lakini ameonyesha kugoma.

“Baada ya kumwandikia barua arudi nyumbani aje kwenye kamati yetu ya maadili, jana wakati akihutubia bunge hilo alisema japo ameitwa na spika, lakini waziri mkuu amemwambia abaki na aendelee na mambo yake, kitu ambacho ni uongo na anatudhalilisha kama nchi. 

 

“Masele ni kiongozi ambaye amekuwa akifanya mambo ya hovyohovyo, ndiyo maana tumemuita atufafanulie huenda yuko sahihi, lakini anafanya mambo ambayo ni hatari kubwa, amejisahau sana, amekuwa akichonganisha mihimili ya Serikali tena ya juu kabisa, hajui hata anatafuta nini.

 

 

Kwa kuwa hataki kuja, nimemwandikia barua Rais wa PAP (Roger Nkodo Dang) ya kusitisha uwakilishi wa Mheshimiwa Masele kwenye bunge la PAP, hadi Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge itakapomalizana naye hapa. Pia, kamati ya maadili ya chama chake (CCM). Kwa hiyo kuanzia sasa siyo mbunge tena wa PAP mpaka tutakapomalizana naye hapa nyumbani,” amesema Ndugai.

Alichokiandika Mhe. Masele leo asubuhi kwenye akaunti yake ya Twitter.

 

TAZAMA ALICHOKISEMA NDUGAI


Toa comment