Breaking: Maalim Seif Afariki Dunia, Maombolezo Siku 7

RAIS wa Zanzibar, Hussein Mwinyi, ametangaza kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, aliyefariki leo Jumatano saa 5:00 asubuhi, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam. Pia ametangaza siku saba za maombolezo.
Akihutubia Taifa kwa njia ya televisheni, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Mwinyi, alisema Maalim Seif alifariki dunia akiwa katika Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa takribani wiki mbili.
”Majira ya saa tano na dakika 26 asubuhi Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad alifariki dunia, Maalim amefariki wakati akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Muhimbili ambapo alikuwa amelazwa tangu tarehe 9 mwezi Februari mwaka huu”. Alisema Rais Hussein Mwinyi.
Rais Mwinyi amesema taifa limepoteza kiongozi mzalendo na shupavu na ametangaza siku saba za maombolezo ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti. Rais Mwinyi amesema taarifa zaidi kuhusu msiba na maziko yake zitaendelea kutolewa na serikali, kwa ushirikiano wa karibu na familia na Chama cha ACT- Wazalendo.
Kwa taarifa zaidi endelea kufuatilia habari zetu kupitia Global APP👇

