The House of Favourite Newspapers

BREAKING: JPM Afanya Ziara Channel 10, Magic FM, Awapa Mamilioni na Mjengo – Video

RAIS wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli leo Jumanne, Februati 5, 2019, ametembelea chombo cha habari cha African Media Group chenye Kituo cha Televisheni cha Channel Ten na Magic FM ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 42 ya kuzaliwa kwa CCM.

 

Wakizungumza na rais katika ofisi za vituo hivyo, wafanyakazi na viongozi wake wamewasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo mishahara midogo na mazingira magumu ya kazi,  jengo chakavu, nia ya kuendelezwa kitaaluma, uhaba wa vifaa,  kukosa bima za afya na mengine mengi.

 

Akijibu changamoto zao, Rais Magufuli amewashukuru wafanyakazi wa vituo hivyo kwa kazi nzuri wanazoendelea kuzifanya na amewahakikishia kuwa yupo pamoja nao huku akiwaahidi kuwapaTsh. Milioni 100 kwa ajili ya ununuzi wa kamera za kisasa, na akaahidi kuwapa Tsh. Milioni 100 ili zitumike katika maboresho ya kituo hicho.

 

Aidha, amewathibitishia kuwa hakuna mfanyakazi atakayefukuzwa na kuwapa uhuru wa kuchagua jengo lolote la CCM kwenye mkoa wowote nchini ili walitumie kama ofisi zao kwa ajili ya uzalishaji wa vipindi na urushaji wa matangazo ili waachane na jengo hilo chakavu wanalotumia kwa sasa.

African Media Group ni moja ya vyombo cha habari vinavyomilikiwa na CCM.

“Ili kuboresha kazi yenu, tutanunua vifaa vipya ili muweze kuwafikia watu wengi sana. Sikujua Channel 10 na Magic FM zinatokea kwenye jengo la ajabu kiasi hiki. Fanyeni utafiti wa majengo ya CCM ili tuangalie wapi tunaweza kuweka ofisi za vituo hivi.Hata mkitaka jengo la Ofisi ya Mwenyekiti wa CCM, mimi nitakubali.  Hata jengo la kupanga tutatafuta, ofisi nyingi zimehamia Dodoma,” alisema akiwaahidi kuwawezesha kupata huduma za matibabu kupitia bima ya afya.

Katika ziara yake hiyo ambayo ilihusiana na kutimia kwa miaka 42 tangu kuzaliwa kwa CCM, aliwataka wafanyakazi wa kituo hicho kuhakikisha kinajitokeza zaidi kikiwa chombo cha chama tawala na kuwaahidi atashirikiana nao katika ufanisi wake.

 

Aliongeza kwa kuwataka wafanyakazi hao kufanya kazi kwa uhuru na kuzingatia maadili ya kazi yao kama ilivyo nchi nzima ambapo kuna vyombo vya habari zaidi ya 170 vilivyosajiliwa nchini.

 

Comments are closed.