The House of Favourite Newspapers

BREAKING: SIMBA YAMTAMBULISHA KOCHA MPYA

Rais wa klabu ya Simba, Salim Abdallah maarufu kama Try Again (katikati) akiangalia kocha wao mpya, Mbelgiji Patrick Aussems akiweka wino kusaini mkataba wa  kuifundisha timu hiyo.

 

UONGOZI  wa klabu ya Simba umemtangaza rasmi kocha wao mpya raia wa Ubelgiji,  Patrick Aussems, ukisema yuko tayari kuanza kazi ya kuiandaa timu kuelekea mashindano ya Ligi Kuu Bara.

 

Simba wameingia makubaliano ya mkataba wa mwaka mmoja na Aussems akiwa anachukua mikoba ya Mfaransa, Pierre Lechantre, ambaye alimaliza muda wake.

 

Hatua hiyo imekuja mara baada ya mabosi wa Simba kugoma kumuongezea mkataba Lechantre ambaye alipewa timu kwa muda wa miezi sita pekee na baada ya kumalizika wakaachana naye.

 

Aussems amesaini mkataba huo mbele ya Makamu wa Rais wa klabu hiyo, Salim Abdallah,  maarufu kama Try Again, sambamba na Kaimu Makamu wa Rais,  Idd Kajuna, na waandishi wa habari.

Kocha huyo amewahi kuzinoa timu kadhaa za Afrika ikiwemo AC Leopards ya Congo, KSA Cameroon ya Cameroon, ES Troyes AC ya Ufaransa na zingine nje ya Afrika.

 

Simba wamefikia hatua ya kumpa mkataba wa mwaka mmoja baada ya kuridhishwa na sifa za kazi yake (CV) zake,  hivyo kuona anastahili kukinoa kikosi hicho ambacho kimeshiriki michuano ya SportPesa Super Cup na Kagame bila ya kuwa na kocha mkuu.

 

Wakati Aussems akimwaga wino, kikosi cha Simba kinatarajiwa kusafiri kuelekea nchini Uturuki kwa ajili ya kambi ya wiki mbili kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa ligi unaotarajiwa kuanza Agosti 22.

Comments are closed.