
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu leo Jumanne Juni Mosi, 2021 amezungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Amesema Idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano kwa shule za Serikali na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi mwaka 2021 imeongezeka kwa asilimia 14.
Ongezeko hilo linakuja baada ya jumla ya watahiniwa waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano kwa shule za Serikali na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi mwaka 2021 kufikia 148,127 kutoka 129,854 mwaka 2020.
Alisema uchaguzi huo umefanyika kwa kuzingatia Takwimu za wanafunzi waliofanya mtihani mwaka 2020 kutoka Tanzania Bara ambapo watahiniwa waliopata daraja la kwanza hadi la tatu walikuwa 153,464 ikiwa wasichana 67,135 na wavulana 86,329, sawa na asilimia 35.06 ya watahiniwa wote.
Alisema kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea waliomaliza kidato cha nne mwaka 2020 wakiwa chini ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ambao walipata daraja la kwanza hadi la tatu walikuwa 479 ikiwa wasichana ni 289 na wavulana 190.

