The House of Favourite Newspapers

BREAKING: ZITTO AFANYA MAAMUZI MAGUMU, AISHIKA PABAYA SERIKALI – VIDEO

KIONGOZI wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe na viongozi wenzake wa vyama vya upinzani nchini, Joran Lwehabula Bashange na Salim Abdallah Rashid Bimani wote wa Chama cha Wananchi (CUF) wamefungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakiiomba mahakama kuzuia Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa kusomwa kwa mara ya pili bungeni kwa madai kuwa unakinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake.

 

Hayo yamesemwa leo na Zitto Kabwe wakati akizungumza na wanahabari katika ofisi za Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) zilizopo, Makumbusho jijini Dar es Salaam.

 

“Serikali imepeleka bungeni muswada wa sheria ya vyama vya siasa unaohalalisha agizo la Rais Magufuli alilolitoa mkoani Singida mwaka 2016 kuzuia mikutano ya vyama vya siasa. Muswada huu unafanya shughuli za kisiasa kuwa suala la jinai.

 

“Tumefungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar chini ya hati ya dharura kupinga Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa kujadiliwa na Bunge kwa minajiri ya kuupitisha kuwa sheria kwa sababu unakinzana na katiba ya nchi. Hatuwezi kwenda kuujadili Bungeni, mnajua kuna wabunge wengi wa CCM, baadhi yao ni wazuri na tumekuwa tukijadiliana nao, lakini wengine ni makasuku.  Kuna wabunge wengine wa CCM wanapenda sifa, siyo kwamba utakuwa mbaya tu lakini utatoka mbaya zaidi.

 

“Muswada huo unalenga kumfanya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa na Mamlaka ya Usimamizi (Regulatory Authority), kuwa na mamlaka ya kuingilia shughuli za kiutawala na maamuzi ya ndani ya vyama vya siasa ikiwemo kusimamisha/ kumfukuza mtu uanachama,” amesema Zitto Kabwe.

 

Aidha, Zitto ameipongeza Mahakama Kuu kwa kutoka katika likizo ili kuja kusikiliza shauri hilo ambalo lilifunguliwa Desemba 20, 2018 na kusajiliwa kama Miscellaneous Civil CaseNo. 31/2018 na imepangwa kutajwa kwa mara ya kwanza kesho, Ijumaa, Januari 4, 2019, mbele ya jopo la majaji ambapo mlalamikiwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

 

Comments are closed.