Bruno amwagia sifa kocha Amorim
Nahodha wa klabu ya Manchester United, Bruno Fernandes (30) amefunguka na kumsifia kocha mpya wa klabu hiyo, Rúben Amorim (39) kuwa ni meneja mzuri mwenye mbinu bora pamoja na uwezo wa kuishi na wachezaji vizuri hivyo ni mtu sahihi wa kukiongozi kikosi hicho kutoka Jiji la Manchester nchini Uingereza.
“Kwangu mimi kinachoonekana kwangu ni uhusiano alionao na wachezaji. Wakati meneja anatoka kwenye klabu yako katikati ya msimu akiwa na vitu vyote vya kushinda, unaona jinsi wanavyomuaga, wanavyomfanya ajisikie kuwa sehemu ya timu na jinsi wanavyomchukulia.
Inaonyesha ni mhusika mkuu na ni mtu anayetoa mchango wake wote kwa wachezaji.” Alisema nahodha huyo katika mahojiano yake na kituo cha televisheni cha klabu hiyo, MUTV.
Fernandes aliongeza kuwa ushawishi wa Amorim unaonekana hasa katika jinsi anavyowakinga wachezaji dhidi ya kukosolewa na kuwaunga mkono kupitia changamoto, tabia, ambayo Fernandes anatumaini Amorim ataleta kitu Old Trafford.
“Nimeona nyakati nyingi ambapo wachezaji walikuwa wakihangaika na anaenda kwenye mkutano na waandishi wa habari kuwatetea wachezaji wake ili kuwapa nafasi nzuri ya kung’ara. Alikuwa na timu changa kwa hivyo alihitaji kufanya hivyo, natumai, anaweza kufanya vivyo hivyo na sisi.”
Fernandes na Amorim hawakuwahi kushiriki chumba cha kubadilishia nguo huko Sporting, kiungo huyo aliondoka katika klabu ya Lisbon na kwenda United kabla ya meneja huyo kuchukua mikoba.
Hata hivyo, kiungo huyo ameangalia kwa mbali mafanikio ya Amorim na anaamini kuwa uhusiano wake na wachezaji unamfanya kuwa kocha mwenye uwezo wa kuleta mafanikio.
Amorim tayari ameshaanza majukumu yake katika viwanja vya Carrington akiwasubiri baadhi ya wachezaji walio katika majukumu ya kimataifa na anatarajiwa kusimama kama kocha mkuu wa klabu hiyo kwa mara ya kwanza Novemba 24 katika mchezo wa Ligi Kuu ugenini dhidi ya Ipswich Town.