The House of Favourite Newspapers

BSS 2015… kilichojificha nyuma ya pazia chafichuka

1

BSS (3)
Madam Ritha akimkumbatia mshindi wa BSS, Kayumba Juma.

Musa Mateja na Imelda Mtema

MASHINDANO ya Bongo Star Search (BSS) 2015, wikiendi iliyopita yalifikia tamati huku historia ya kwanza ikiwekwa na kijana mwenye umri wa miaka 19 tu, Kayumba Juma aliyeibuka kidedea kwa kuwatupa wenzake 6 waliofaulu kuingia fainali na licha ya shughuli hiyo kumalizika salama, lakini kilichojificha nyuma ya pazia kimefichuka.

BSS (5)Fainali hizo zilifanyika Oktoba 9, mwaka huu kwenye Ukumbi wa King Solomon uliopo Ada Estate, Kinondoni jijini Dar huku zikishuhudiwa na maelfu ya wakazi wa jiji, burudani zilikuwa kibao siku hiyo ambapo zilianza saa 3: 30 usiku zikifunguliwa na mkali wa miondoko ya R&B, Bongo,  Bernard Paul ‘Ben Pol’.

BSS (1)WASHIRIKI WAANZA

Baada ya Ben Pol kufungua ukurasa huo, kete ya kwanza kwa washiriki ilianza kwa kumdondokea mshiriki kutoka Mwanza, Angel Mary Kato aliyeonesha manjonjo yake  akimpisha Kayumba Juma ambaye aliingia na Wimbo wa  Christian Bella huku akipata shangwe nyingi kutoka kwa mashabiki waliomtunza fedha.

BSS (2)
Baadaye, Nasibu Fonabo akichukua nafasi ya tatu kwa kufungua jukwaa hilo, tena akitumia gitaa huku Kelvin Geryson akiingia kwa makeke mengi na kumpisha Frida Amani ambaye alikuwa mshiriki kutoka Kaskazini.

Jackline Kakengi kutoka Bukoba alitoka na kuacha washiriki wenzake wakisonga mbele na kuunda Tano Bora.

bssLAKINI SASA

Hata hivyo, ukiachana na ushindi huo wa Kayumba, kuna mambo ambayo yalizua gumzo ukumbini hapo ambapo u-team wa majaji. Wasanii waligawanywa katika makundi ya Madam Ritha, Salama Jabir na Master J na kuonekana wazi hasa pale mshiriki wa jaji mmojawapo alipokuwa akipongezwa tofauti na ilivyokuwa kwa yule ambaye si wa timu yake, jambo lililolalamikiwa na mashabiki.

Mashabiki wengi walisema, siku ya fainali, majaji hao ‘wanaojua kusema’ wangekuwa kimya kama inavyokuwa kwenye shindano la Miss Tanzania.

MFANO NI SALAMA

Katika kipengele hicho cha u-team, jaji Salama Jabir alionesha mapenzi yake waziwazi kwa Kayumba baada ya kumsifia kutokana na kupafomu Wimbo wa Aisha Ramadhan ‘Isha Mashauzi’ katika raundi ya mwisho.

Salama alisema: “Bwana wee gitaa kitu gani? Sisi watu wa uswahilini bwana, tuna mambo yetu na hayo mambo ya gitaa kwanza hatujayazoea, hongera Kayumba.” (akimaanisha kuwa, Nasibu Fonabo hakufanya kitu baada ya kupafomu na gitaa).

BSS (4)MASHABIKI WASEMA KAYUMBA ALIANDALIWA

Baada ya ushindi huo wa Kayumba, gumzo kubwa liliibuka mashabiki ukumbini hapo wakidai kuwa aliandaliwa mapema kutwaa taji hilo kwa msimu huu kwani baadhi ya kura zilionesha mapema.

“Bwana wee, yaani hapa ni kama tumeliwa. Inaonesha kuwa nyuma ya pazia Kayumba aliandaliwa toka kitambo awe mshindi kwani utaona hata majaji wenyewe, kama Salama  alionesha wazi mapenzi yake kwa mshiriki huyo,” alisema mmoja wa wahudhuriaji.

KUNA UPENDELEO WA WANAUME?

Katika hatua nyingine, baadhi ya mashabiki walisema mashindano hayo yametawaliwa na uchaguzi wa wanaume tu licha ya muandaaji wake kuwa mwanamke.

Walisema mpaka juzi, BSS imetimiza misimu nane huku sita ikitwaliwa na wanaume tu, jambo lililotafsiriwa kuwa huenda waandaaji wake hawazingatii usawa.

KUMBUKUMBU YA WIKIENDA

Ilibidi gazeti hili lifukue kwenye kumbukumbu zake za nyuma na kubaini kwamba, washiriki waliowahi kutwaa taji hilo tangu kuanzishwa mwaka 2006 ni Jumanne Idd (mwanaume), Pascal Casian (mwanaume), Emmanuel Msuya (mwanaume), Misoji Nkwabi (mwanamke), Walter Chilambo (mwanaume), Mariam Ramadhan (mwanamke), Haji Ramadhan (mwanaume)  na sasa Kayumba Juma (mwanaume).

UKUMBI PIA WAZUA MANENO

Baadhi ya mashabiki walisema kutokana na mashindano hayo kuwa makubwa, yangefanyiwa kwenye ukumbi mkubwa zaidi kama ilivyozoeleka kuliko kupeleka sehemu ngeni.

MADAM NA GAUNI LA BEI MBAYA

Lingine lililozua gumzo ukumbini, ni Madam Ritha kuvaa gauni ambalo lilikadiriwa kuuzwa dukani kwa shilingi laki tano.

Ijumaa Wikienda lililazimika kumfuata Madam kwa lengo la kujua bei ambapo alisema alilitungua dukani kwa shilingi milioni moja na laki nane (1,800,000).

1 Comment
  1. […] wa nne wa michuano ya Bongo Star Search (BSS) ya mwaka 2015, Angel Mary Kato, amerudi upya kwenye gemu ya Hip Hop na ameachia ‘audio’ ya kibao […]

Leave A Reply