The House of Favourite Newspapers

Bukoba: Kesi ya Walimu Kumuua Mwanafunzi Yaanza Kusikilizwa

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Bukoba imeanza kusikiliza kesi ya mauaji ya kukusudia jana inayomkabili Mwalimu Herieth Jerald wa shule ya msingi Kibeta iliyoko Manispaa ya Bukoba.

 

Mwalimu huyo pamoja na mwenzake, Respicius Patrick,  wanadaiwa kutekeleza mauaji ya mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo marehemu Sperius Eradius aliyekuwa na umri wa miaka 14, akimtuhumu kuiba pochi yake.

 

Katika kesi hiyo, mwanafunzi huyo anadaiwa kuuawa na walimu hao kwa kupigwa Agosti 27 mwaka jana, akidaiwa kuiba pochi ya mwalimu Heriet Jerald baada ya kumpokea mizigo wakati akiingia kazini.

 

Mahakama imeelezwa na mwendesha mashtaka kiongozi wa serikali, Chema Maswi,  kuwa washtakiwa hao walimuua kwa kukusudia mwanafunzi huyo katika eneo la shule ya msingi Kibeta, ambapo washtakiwa walikana mashtaka hayo.

 

Mshtakiwa mmoja kati ya sita waliokuwa wameletwa mahakamani hapo, Benidius Benezeth, ambaye ni mwendesha pikipiki aliyemsafirisha mwalimu  Jerald alitoa ushahidi dhidi ya mwalimu huyo na kudai kuwa wakati akimsafirisha hakuona kama katika kikapu alichokuwa amebeba kuna pochi maana hakukikagua.

 

Baada ya kesi hiyo kuaihirishwa hadi Februari 08 mwaka huu, ushahidi utakapoendelea kutolewa, mwendesha mashtaka, Maswi ameeleza mwenendo wa kesi hiyo kwa upande wa serikali.

Comments are closed.