The House of Favourite Newspapers
gunners X

Bukuku Bahati Ampa Nandy Sharti la Kuokoka!

0

UNAPOUZUNGUMZIA muziki wa Injili Bongo, huwezi kuacha kumtaja nguli wao ambaye ni mwanamama kutoka mkoani Mbeya, Bahati Bukuku.

Ni mmoja wa wakongwe kwenye muziki wa Injili, mwenye sauti ya kipekee aliyojaaliwa na Mungu.

 

Bahati kama jina lake lilivyo, amepata umaarufu mkubwa kutokana na uimbaji wa nyimbo zake ambazo zimekuwa na maneno yanayogusa jamii ipasavyo.

Miongoni mwa nyimbo zake kali ni pamoja na Dunia Haina Huruna, Majaribu, Ni Nyakati za Mwisho, pamoja na Nakutegemea.

 

Leo katika makala haya, Bahati amefunguka mengi ikiwemo sababu ya yeye kuwa kimya kwa muda mrefu, twende pamoja:

Risasi: Upo kimya sana kwa muda mrefu haujatoa wimbo wowote, tatizo ni nini hasa?

 

Bahati: Ni kweli nilikuwa kimya sana, ila kwa sasa hivi nimeshaandaa nyimbo na nimesharekodi, nasubiri muda ufike ili niweze kuziachia.

Risasi: Muziki wa Injili umeuanza muda mrefu sana, tunaweza tukasema wewe ndiyo njia ya wengine wanaokuja. Je, kuna tofauti gani kati ya nyimbo za Injili za sasa hivi na zile za zamani?

Bahati: Mimi nadhani hakuna tofauti yoyote kwa sababu muziki ni uleule, kwa hiyo mabadiliko yaliyopo ni ya kawaida kwa sababu lazima muziki ukue na hata tulivyokuwa tunaimba sisi, tuliowakuta walikuwa wanaimba tofauti, ila na sisi tukauboresha kwa hiyo hata hawa wanatakiwa watafute style yao wenyewe ili uzidi kuwa mzuri.

Risasi: Wanaoimba nyimbo za Injili ni tofauti na wanavyoishi kabisa, yaani wewe kwa upande wako unalizungumziaje suala hili?

 

Bahati: Hayo ni maamuzi ya mtu mwenyewe, binafsi kwa sababu suala la mtu ni kitu gani anachokiishi, anakijua mwenyewe. Kwa hiyo, suala la mtu kuimba tofauti na anachokiishi ni mtazamo wake mwenyewe.

Risasi: Ni msanii gani wa Bongo Fleva ambaye unamuona ana muonekano mzuri wa kumuimbia Bwana Yesu na unatamani abadilike aachane na nyimbo hizo za kidunia na amtumikie Mungu?

 

Bahati: Mimi nadhani ni wasanii wote wa Bongo Fleva wanatakiwa waachane na nyimbo za kidunia na warudi kwa Mungu wao kwa sababu hizi ni nyakati za mwisho, lazima tumuombe na kumuabudu Mungu.

Risasi: Sasa hivi limejitokeza suala la wasanii wengi wa Bongo Fleva kuimba kava za muziki wa Injili kama Nandy, Ben Pol na wengine. Wewe kwa mtazamo wako unahisi ni jambo zuri wanalolifanya?

 

Bahati: Unajua kama waimbaji wa Injili wangekuwa wanaimba Bongo Fleva, hapo ndipo ningekuwa na la kuongea lakini kama Bongo Fleva wanaimba Injili, mimi wala sishangai kwa sababu naona ni neema ya kuelekea kwenye wokovu.

 

Risasi: Unaamini kiki kwenye muziki wa Injili?

Bahati: Jamani mimi siamini kiki kabisa kwa sababu naamini neema ya Mungu inatosha kabisa, kiki ni kujishushia hadhi.

 

Risasi: Tofauti na muziki wa Injili, unajishughulisha na kitu gani kingine?

Bahati: Mimi ni mfanyabiashara, nina biashara zangu nyingi tu nafanya lakini nisingependa kuziweka wazi kwa sasa.

 

Risasi: Siku moja ikitokea msanii wa Bongo Fleva, Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’ akaja akahitaji kuimba na wewe muziki wa Injili, je utakubali kuimba naye?

Bahati: Labda aokoke, akiokoka inawezekana lakini kama hataki kuokoka basi mimi sitaweza kufanya hivyo.

 

Risasi: Ahsante sana ubarikiwe.

Bahati: Amina, na wewe pia barikiwa!

MAKALA: Khadija Bakari, Risasi

Leave A Reply