The House of Favourite Newspapers

BUNGE LA RIDHIA ITIFAKI YA ZIADA YA NAGOYA – KUALA LUMPUR

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. George Simbachawene akiwasilisha azimio la Itifaki ya ziada ya Nagoya – Kuala Lumpur juu ya uwajibikaji wa kisheria na fidia kwa madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa mbele ya Bunge hii leo mjini Dodoma. Ni itifaki itakayosaidia juhudi za kuhifadhi mazingira na matumizi endelevu ya bioanuai kwa kutambua madhara yanayoweza kutokea katika afya ya binadamu, mazao au bidhaa zilizofanyiwa mabadiliko ya kijenetiki kwa njia ya bioteknolojia ya kisasa.

Bunge la Tanzania hii leo limeridhia Itifaki ya ziada ya Nagoya – Kuala Lumpur juu ya uwajibikaji wa kisheria na fidia kwa madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa.

 

Akiwasilisha azimio Bungeni Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) George Simbachawene amesema kuridhiwa kwa Itifaki hiyo, Tanzania itaimarisha ushirikiano na Nchi Wanachama katika kusimamia na kutekeleza masuala yanayohusu bidhaa au mazao ambayo yanatoka nje ya Nchi.

 

Aidha, imebainika kuwa Itifaki ya Nagoya – Kuala Lumpar itasaidia juhudi za kuhifadhi mazingira na matumizi endelevu ya bioanuai kwa kutambua madhara yanayoweza kutokea katika afya ya binadamu, mazao au bidhaa zilizofanyiwa mabadiliko ya kijenetiki kwa njia ya bioteknolojia ya kisasa.

 

Simbachawene amesema kuwa Itifaki hii itaongeza upatikanaji wa fursa za kujenga uwezo wa wataalam nchini katika kusimamia matumizi salama ya bioteknolojia ya kisasa na kusimamiwa na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni za Usimamizi wa Matumizi Salama ya Bioteknolojia ya Kisasa ya Mwaka 2009.

 

“Itifaki ya Nagoya – Kuala Lumpar itasaidia kuimarisha uhifadhi wa mazingira, kulinda afya ya binadamu na wanyama dhidi ya madhara yatokanayo na matumizi ya bioteknolojia ya kisasa” alisisitiza Simbachawene.

 

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Kanali (Mst) Masoud Ali Khamis ameishauri Serikali kuzipitia Sheria za nchi ambazo zitaenda sambamba na malengo ya Itifaki kwa kuhakikisha nchi inanufaika.

 

Itifaki ya Ziada ya Nagoya – Kuala Lumpur kuhusu uwajibikaji kisheria na fidia kwa madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa ilianzishwa ili kuwezesha utekelezaji wa Itifaki ya Cartagena inayohusu Matumizi Salama ya Bioteknolojia ya Kisasa ilipitishwa na Nchi Wanachama wa Mkataba wa Hifadhi ya Bioanuai Mwaka 2000 ambapo Tanzania iliridhia Itifaki hii mwaka 2003.

Comments are closed.