BUNGE limeazimia na kupitisha mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge ambapo limemsimamisha Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema (Chadema) kuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge kuanzia leo Aprili 4, 2019, hadi Januari 2020, kwa kuunga mkono kauli ya kuwa ‘bunge ni dhaifu’.
Akiwasilisha hoja hiyo Bungeni mwenyekiti wa kamati hiyo EMANUEL MWAKASAKA amesema kuwa Mbunge huyo alipopewa nafasi ya kujitetea kwenye kamfati alisema ahukumiwetu kwani alichozungumza ni kweli.
Spika wa bunge Job Ndugai amemtahadharisha Lema kuwa pamoja na adhabu aliyopewa na Bunge huko aliko akiendelea kulidhalilisha Bunge ataitwa tena kwenye kamati ya haki kinga na madaraka ya Bunge na kuhojiwa.
Baada ya maamuzi hayo, Wabunge wa upinzani wamesusa na kutoka nje ya kikao cha bunge kinachoendelea mjini Dodoma wakipinga maamuzi hayo. Ndugai pia amewaagiza maaskari wa Bunge kuhakikisha wabunge wote waliosusia kikao cha Bunge na kutoka nje hawarudi Bungeni tena kwa siku ya leo.
Mbunge huyo kupitia akaunti yake ya Twitter ameandika; Nimesimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge mpaka January 2020. Moyo wangu una amani sana, kwani mahusiano yangu na HAKI yanaendelea kuimarika zaidi. Nawatakia Wabunge wenzangu kazi njema katika wajibu huu, sitanyamaza hata kama adhabu itakuwa ni mauti.


Comments are closed.