The House of Favourite Newspapers

Bunge latikisika, wapinzani watimuliwa

0

TOKA1Na Elvan Stambuli
BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo alasiri limetikisika baada ya wabunge wa upinzani kuwazomea viongozi wa Serikali ya Zanzibar walipokuwa wakiingia bungeni.

Wa kwanza kuzomewa alikuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Kificho na baadaye Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Balozi Seif Idd walipokuwa wakiingia ndani ya bunge hilo ambapo wabunge wa kambi ya upinzani licha ya kutakiwa kusimama, waliketi.

Kama vile hiyo haitoshi, wabunge hao wa upinzani walianza kupiga meza zao huku wakisema “Maalim Seif, Maalim Seif, Maalim Seif.”
Awali aliyekuwa Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani katika bunge lililopita, Tundu Lissu alimuomba Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson mwongozo wa spika, hata hivyo, alikataliwa.

Baadaye ikaja zamu ya kuingia bungeni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, hali ikawa mbaya zaidi kwa wabunge wa kambi ya upinzani kuzomea huku wakiimba ‘Maalim Seif’, hali iliyomfanya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuwanyamazisha bila mafanikio.

Kuona hivyo, Spika Ndugai aliwaamuru wabunge hao wa upinzani kutoka nje. “Waheshimiwa wabunge nawaombeni kwa hiari yenu mtoke nje ya ukumbi wa bunge,” alisema Spika Ndugai, hali iliyowafanya wapinzani hao kunyanyuka vitini mwao na kutoka nje ya Bunge.

Mbunge pekee wa upinzani ambaye hakutoka ukumbini ni Zitto Kabwe wa Jimbo la Kigoma Mjini ambaye baadaye alipongezwa na Rais John Pombe Magufuli ambaye mara tu baada ya kufika katika viwanja wa vya bunge, alikagua gwaride la polisi lililoandaliwa kwa ajili yake.

Mara baada ya wabunge wa upinzani kutoka ukumbini, Spika Ndugai alimkaribisha Rais Magufuli kulihutubia Bunge hilo na hadi wakati naandika habari hii saa 10 na dakika 36 jioni kiongozi huyo wa nchi anaendelea kuhutubia Bunge.

Leave A Reply