The House of Favourite Newspapers

Busungu Autafuta Utajiri kwa Kilimo cha Vitunguu, Ufugaji

0

UKIZUNGUMZIA nyota wa zamani katika kipindi cha hivi karibuni, huwezi kumsahau aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Malimi Busungu ambaye aliwika sana na kikosi hicho mara baada ya kusajiliwa.

 

Awali, Busungu alitua Yanga mnamo mwaka 2015 akitokea Mgambo JKT ambapo ni miongoni mwa nyota ambao usajili wao ulitikisa kufuatia kugombaniwa na vigogo wawili, Simba na Yanga ambapo mwisho wa mchezo akatua Jangwani kwa mkataba wa miaka miwili.

 

Mshambuliaji huyo hakuweza kutamba sana katika soka la Bongo ambapo awali alianza kuzitumikia timu za Polisi Moro, Villa Squad, Coastal Union, Kagera Sugar, Mgambo JKT, Yanga na baadaye Lipuli.

 

Busungu ambaye aliitumikia Yanga kwa misimu miwili, alitimka katika kikosi hicho mwaka 2017 baada ya kuitumikia kwa misimu miwili na kujiunga Lipuli ya Iringa ambapo ndipo alipokwenda kumalizia maisha yake ya soka.

 

Wakati alipokuwa akiichezea Yanga, Busungu aliwahi kuingia katika mgogoro na aliyekuwa kocha msaidizi enzi hizo, Juma Mwambusi chini ya kocha, Hans van Der Pluijm kwa madai kuwa ndiye aliyekuwa chanzo cha yeye kutopangwa katika kikosi hicho na mwisho wake kuonekana hana uwezo na kufungashiwa virago.

 

Championi Jumatatu limepata nafasi ya kuzungumza na Busungu ili kujua yupo wapi kwa sasa na nini anafanya baada ya kuachana na mpira.

 

ILIKUWAJE UKAO NDOKA YANGA?

“Nilia chana na Yanga kwa kuwa mkataba wangu na klabu hiyo ulikuwa umekwisha. Hakukuwa na mazungumzo mengine, hivyo nikaamua kwenda katika timu nyingine.

 

KWA NINI ULIKWENDA LIPULI?

“Nilijiunga na Lipuli Julai 2017, niliona ni miongoni mwa timu bora ambazo zilikuwa zikichipukia na kufanya vizuri kwenye ligi, awali wakati natua katika timu hiyo, mambo yalikuwa mazuri lakini msimu wa pili mambo yalibadilika kufuatia aliyekuwa mwenyekiti wa timu hiyo, Ramadhani Maano kuondoka ambaye alikuwa akisikiliza sana wachezaji hasa katika suala la maslahi, lakini alivyoondoka yeye mambo yakawa ndivyo sivyo na ndio sababu ya kuondoka.

 

KWA NINI ULIAMUA KUACHANA NA MPIRA MAPEMA?

“Malipo ndio yaliyosababisha nikate tamaa ya kuendelea kucheza mpira na kuamua kuachana na kazi hiyo kutokana na kuona jambo la maslahi ni gumu kutimizwa katika baadhi ya klabu za ligi kuu, hivyo nikaona nifanye shughuli nyingine yenye kunipatia maslahi.

 

“Nimeamua kuangalia upande mwingine kwa kukomaa na maisha ya uswahilini kwa kuondokana na soka, hivyo kuja kupambana upande huu ili nione mafanikio yake.

 

JE, UNAWEZA KURUDI TENA KWENYE SOKA?

“Kwa jinsi nilivyo hivi sasa ni vigumu kwa upande wangu kurudi katika maisha ya soka na badala yake naangalia shughuli zangu zaidi zinazoniingizia kipato kwa ajili ya maisha yangu ya baadaye, huko kwenye mpira nimeshapita hivyo kwa sasa basi.

 

UNAJISHU GHULISHA NA NINI?

“Nimeanza kwa kujishughulisha na kilimo cha vitunguu huku Bariadi (mji uliopo mkoani Simiyu), mradi ambao naona unanilipa kwa kiasi fulani kutokana na jinsi ninavyoyaona matokeo.

“Kilimo cha vitunguu ni miongoni mwa kilimo bora hasa msimu ukiwa mzuri kwani kila msimu una mabadiliko yake na bei hupanda kulingana na msimu husika.

 

UMEANZA LINI KULIMA VITUNGUU?

“Baada ya kutoka kwenye mpira ndiyo nikaamua kugeukia huku, sina muda mrefu na sitegemei kuachana na kilimo hiki na kwa sasa nipo katika harakati za kutafuta manufaa ya kilimo cha vitunguu.

 

UNALIMA HEKA NGAPI?

“Kilimo cha vitunguu pia kinategemea na mfuko wako upoje, kama eka moja, mbili, tatu na kuendelea kulingana na fedha ulizonazo, hivyo nalima kulingana na mfuko wangu kwani ulimaji wa vitunguu una gharama.

 

UMEPATA MAFANIKIO GANI KATIKA KILIMO CHA VITUNGUU?

“Kwa sasa mimi ni mkulima mchanga, sijapata mafanikio bado.

 

MAUZO YA VITUNGUU KWA JUMLA YAPOJE?

“Faida ya vitunguu inategemea na msimu husika, kwani kila msimu una bei yake kutegemea na uhitaji wa vitunguu kwani katika siku za hivi karibuni bei ya vitunguu ilipanda sana.

 

“Kwa mfano juzikati bei ya vitunguu ilikuwa juu gunia moja ilikuwa laki tano, na vikiwa vingi bei inapungua na kuuzwa kwa bei ya kutupa, hivyo wakulima wanakuwa hawapati kitu ambapo gunia linaweza kuuzwa kuanzia elfu 70, 90, 80 na laki moja.

 

JE, UNATARAJIA KUANZISHA LINI MRADI WA UFUGAJI?

“Nahitaji kujiendeleza zaidi kwa kuanzisha ufugaji wa kuku wa kisasa pamoja na ufugaji wa nguruwe, naamini watanisaidia kuweza kupanua kipato changu.

 

“Shughuli za ufugaji nahitaji kuzianzisha Dodoma ambapo tayari nimeshaandaa mabanda kwa ajili ya kazi hiyo ambayo nitaianza wakati wowote kuanzia sasa.

“Kuna mabanda ya kuku nimeshayatengeneza pamoja na ya nguruwe ambao tayari wameshaanza kuwekwa wachache na natarajia kuwaweka wengine zaidi.

 

UNATUMIA MTAJI WA KIASI GANI KUANZISHA MRADI WA UFUGAJI?

“Sina kiwango maalumu inategemea na kiasi nilichonacho kwa wakati husika, hivyo nitaanza na mtaji kiasi nilionao na biashara ikiwa nzuri zaidi ndipo nitakapojipanua kwa kuwa na mtaji mkubwa zaidi.

 

UNAZUNGUMZIAJE YANGA YA CEDRIC KAZE?

“Msimu huu imebadilika, mwanzo ilikuwa inayumbayumba, kwa sasa imeanza kukaa sawa, mpira ni mazoezi, ujio wa kocha Kaze utasaidia kuweza kukiimarisha kikosi chao na kufanya vizuri msimu huu.

 

UNAIZUNGUMZIAJE SIMBA YA SASA?

“Ligi bado ipo, lolote linaweza kutokea, kwani hadi sasa huwezi kutabiri nani atakuwa bingwa kwa kuwa mechi bado zipo nyingi sana, Simba imeteteleka katika mechi zake za awali lakini naamini watakuja kukaa sawa.

 

UNA USHAURI GANI KWA WACHEZAJI WALIOBWETEKA BAADA YA KUACHANA NA SOKA?

“Waangalie maisha baada ya mpira ni jukumu lao, kwani mpira wanacheza kwa muda mchache sana ukilinganisha na maisha baada ya mpira ambayo ndiyo tunayaishi kwa muda mrefu.”

KHADIJA MNGWAI, Dar es Salaam

Leave A Reply