KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Pius Busitwa, leo atacheza namba tisa akimrithi mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa aliyeshindwa kuongozana na msafara huo kuelekea Shelisheli.
Kutokana na ushindi wa bao 1-0 Jijini Dar es Salaam, Yanga leo inahitaji suluhu, sare, ushindi na hata ikifungwa mabao 2-1 itasonga mbele kwenye hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mzambia huyo aliachwa katika msafara huo kwa kile kilichodaiwa kupata maumivu ya misuli ingawa habari zingine zinadai kwamba hayuko sawa na viongozi.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, Kocha Mkuu Mzambia, George Lwandamina, ameanza kumuandaa Buswita kucheza nafasi hiyo katika mazoezi ya siku ya kwanza tangu wamefika nchini
Kwa mujibu wa programu za mazoezi ya Lwandamina, Buswita amekuwa akicheza nafasi hiyo ya ushambuliaji wa kati namba tisa, nyuma yake namba kumi atacheza Ibrahim Ajibu tangu Yanga ilipoanza programu mjini hapa.
Awali Buswita alikuwa akitumika kama namba saba lakini benchi la ufundi limeangalia na kujiridhisha kwamba ndiye mchezaji pekee anayeweza kuongeza kasi ya mashambulizi ndio maana wakamhamisha.
Katika mazoezi yaliyofanyika mchezaji huyo alionyesha uwezo mkubwa kwenye kupachika mabao na kutengeneza nafasi ambazo zinamfaa sana Ajibu haswa kwa aina ya matokeo Yanga inayosaka leo Jumatano.
Meneja mkuu wa timu hiyo, Hafidh Saleh alipoulizwa kuhusu hilo alisisitiza kuwa; “Kocha anawaandaa baadhi ya wachezaji watakaochukua nafasi ya Chirwa kucheza nafasi yake na kati ya hao yupo Buswita. Tangu tumefika hapa Shelisheli katika mazoezi yake kocha wetu Lwandamina amekuwa akimpanga Buswita kucheza namba tisa na chini yake namba kumi anacheza Ajibu, hivyo ninaamini wachezaji hao watacheza pamoja katika nafasi hiyo.”
Hafidh ambaye ni miongoni mwa wanachama waandamizi wenye heshima kubwa ndani ya Yanga, aliongeza kwamba kwa hali iliyo lazima washinde mchezo huo bila wasiwasi.
Comments are closed.