Bwalya Akomba Milioni 138 Simba SC

KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Mzambia, Larry Bwalya, ameikamua timu hiyo Sh milioni 138 kama ada ya usajili akisaini mkataba wa miaka miwili.

 

Bwalya amejiunga na Simba akitokea Power Dynamos inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia akiwa mchezaji wa pili kutoka taifa hilo kuichezea Simba baada ya Clatous Chama.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Spoti Xtra limezipata ni kuwa, kiungo huyo amekubali kujiunga na Simba baada ya makubaliano ya kupatiwa dola 60,000 (sawa na Sh 138,565,000) kama sehemu usajili wake.

 

“Bwalya yeye amejiunga na Simba kwa dau la dola 60,000 kutokana na makubaliano yake, timu na wakala ambaye amesimamia dili hilo hadi amejiunga na Simba.

 

“Nadhani hiyo siyo pesa ndogo kwa sababu ukiangalia ni zaidi ya milioni mia, naamini atakuwa msaada ndani ya Simba hasa kutokana na uwezo wake kuwa mkubwa, lakini akiwa ni mchezaji chaguo la kwanza ndani ya kikosi cha Zambia,” kilisema chanzo chetu.

Toa comment