The House of Favourite Newspapers

Bwana Harusi Aliyeingia Mitini: Shetani Alinipitia

1

Mayasa Mariwata na Gabriel Ng’osha | Gazeti la AMANI, Toleo la Desemba 22, 2016

DAR ES SALAAM: Katika kile kinachoonekana ni kioja cha kufungia mwaka baada ya bwana harusi Samuel John Mwakalobo kutofika kanisani kufunga ndoa na mwandani wake, Given Michael Mgaya, mwanaume huyo ameongea na Amani na kusema shetani alimpitia.

Hata hivyo, kwa mujibu wa chanzo chetu ndani ya familia hiyo, mwanaume huyo mwanzo alikuwa na utayari wa kufunga ndoa lakini cha ajabu siku hiyo ya ndoa iliyotakiwa kufungwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania  (KKKT), Isanga mkoani Mbeya ikifuatiwa na sherehe katika Ukumbi wa Mkapa Conference Center- Sokomatola jijini humo, aliingia mitini.

 “Jambo hilo limezua kioja kwa kweli. Hata wanafamilia wapo njia panda. Hata hivyo, yule mwanaume akiulizwa chanzo cha kutofika kufunga ndoa anashindwa kueleza vya kueleweka, wakati alionesha ushirikiano mzuri, inawezekana kuna taarifa alipata zikamfanya asite,” kilisema chanzo.

Baada ya kupata taarifa hizo, paparazi wetu alimtafuta mwanaume huyo ambaye alisema kuwa hataki kuongelea masuala hayo hadi atapokuwa tayari, lakini paparazi wetu alipomtupia maswali ya rasharasha alijikuta akijibu bila matarajio ambapo alisema haelewi nini kilitokea, huenda alifanyiwa mambo ya kishirikina kwa sababu anampenda sana mchumba wake huyo.

“Mimi mwenyewe sijui nini kilitokea maana mke wangu nampenda hakuna chochote alichonikosea na si kwamba kuna mtu mwingine nampenda ndo’ maana nikaghairi kumuoa yeye, huenda nilifanyiwa miujiza ila Mungu ndo’ anajua yote.

“Sijui hata yeye amelipokeaje hilo suala, ila kuhusu ishu ya ndoa mpaka sasa nimemkabidhi Mungu. Kifupi ni shetani alinipitia kukacha kwenda kufunga ndoa na siyo kwamba nilibaini anachepuka,” alisema.

Hata hivyo, shushushu wetu aliamua kumtafuta mwenyekiti wa kamati ya harusi hiyo ambaye alieleza kuwa, wao hawana wanachojua, wakimuuliza mwenyewe hajielewi, ila  anachowajibu ni kwamba bado anampenda bibi harusi, huenda alirogwa.

“Mbona Send Off iliyofanyika Kimara Dar  alishiriki vizuri, iwenje ndoa? Huenda alipitiwa na upepo mbaya, japo ndoa haikufungwa. Tulifanya sherehe kwa kuwa tulikuwa tumeshagharamia ukumbi, vinginevyo ingetulazimu kuwarudishia watu pesa zao walizochanga. Sherehe hiyo haikuhudhuriwa na bibi harusi, bwana harusi wala ndugu wa mke,”alisema.

Kwa upande mchungaji ambaye alipaswa kufungisha ndoa hiyo, Andangile Mwakijungu baada ya kuulizwa na paparazi wetu alisema:

“Mimi ninachojua, hawa watu wameongea wameyamaliza. Mimi nawasikiliza wao tu maana walishakuja kuandikisha ndoa kanisani. Wakitaka kufunga sawa. Nasikia bwana harusi ameshakwenda kwa wakwe zake kuongea nao, wameyamaliza.”

Comments are closed.