The House of Favourite Newspapers

Bweni Lililochomwa 2018 Laungua Tena, Kura Zapigwa ‘Kubaini’ Wahusika

0

 

SEHEMU ya bweni la wavulana wa Shule ya Sekondari Mang’oto wilayani Makete mkoani Njombe, imeungua moto na kusababisha hasara ya baadhi ya vifaa vilivyokuwemo katika bweni hilo.

 

 

Mkuu wa Wilaya ya Makete, Veronika Kessy, ametembelea  shule hiyo na kusikitishwa na tukio hilo ikizingatiwa kuwa bweni hilo liliwahi kuungua kwa kuchomwa moto na mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo mwaka 2018 na ameagiza kuchukuliwa hatua mara moja.

 

 

“Nilipopokea taarifa za kuungua kwa bweni la Mang’oto nimepatwa na mfadhaiko kwa sababu bweni hili liliungua mwaka 2018 mwezi Machi na tukafanya jitihada kubwa kuchangisha wananchi na wadau ili  kutoa fedha na kurudisha hili bweni sehemu yake, sasa katika kipindi cha miaka miwili bweni linaungua tena katika mazingira yale yale,” alisema Kessy.

 

Kamati ya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na maafisa wengine wa serikali wamefika katika shule hiyo ambapo katika hatua za awali limeendeshwa zoezi la kupiga kura ili kuwabaini wahusika na baada ya zoezi hilo kamati hiyo imeondoka na wanafunzi kadhaa kwa mahojiano zaidi.

 

 

Kessy amesema hatua hizo ni za awali huku akiwataka wanafunzi wanaowafahamu waliofanya kitendo hicho kutoa ushirikiano kupitia kwa walimu wao.

 

 

“Kama kuna mtu mnamfahamu amefanya hicho kitendo mumfuate mwalimu wa malezi;  nenda ukamwambie ,itakuweka huru,” aliwaeleza wanafunzi. Afisa Elimu Mkoa wa Njombe,  Mwalimu Gift Kyando, amewaeleza wanafunzi kutambua wajibu wao wawapo shuleni.

 

 

“Ukasirike vyovyote lakini si kuchoma bweni wala kuchoma darasa, ninyi mmechoma bweni mara ya pili sasa,wazazi wenu huko wanahangaika wewe unachoma mahali pa kulala!”aliwaambia wanafunzi.

 

 

Afisa elimu wa kata hiyo, Furaha Kyando, amemteua Mwalimu Jacob Mdibwa kusimamia shule kwa kipindi ambacho uchunguzi unaendelea juu ya tukio hilo.

 

 

Leave A Reply