The House of Favourite Newspapers

Caf Yaiongezea Nguvu Yanga

SHIRIKISHO la Soka Afrika (Caf), limewafahamisha Yanga kuwa wataweza kuwatumia wachezaji wao wa kimataifa mshambuliaji, David Molinga na beki Mrundi, Moustafa Selemani.

 

Hiyo ni furaha kubwa kwa mashabiki wa Yanga ambao sasa watakuwa na silaha zao zote kuelekea mchezo wa mtoano wa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids FC ya nchini Misri.

 

Mchezo huo umepangwa kucheza Oktoba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza. Na sasa Yanga wataingia wakiwa na imani kubwa.

 

Molinga ameifungia Yanga mabao mawili kwenye Ligi Kuu Bara hadi sasa.

Awali, wachezaji hao walikosa leseni kutoka Caf, hivyo hawakuwahi kuitumikia klabu hiyo kwenye michuano ya kimataifa kutokana na usajili wao kuchelewa.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu na kuthibitishwa na Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, tayari wamepokea taarifa hiyo kutoka Caf ikiwafahamisha wataweza kuwatumia nyota wao hao.

 

Mwakalebela alisema kuwa ni taarifa nzuri kwao katika kukiimarisha kikosi chao kuelekea mchezo wao mgumu dhidi ya Pyramids ambao wamepanga kupata matokeo mazuri ya ushindi nyumbani kabla ya kwenda ugenini.

 

Aliongeza kuwa hivi sasa wanasubiria kibali hicho rasmi kutoka Caf kitakachofika wakati wowote Yanga tayari kwa ajili ya kuwatumia wachezaji hao muhimu.

“Caf ipo kwenye hatua za mwisho za kutupatia kibali cha Molinga na Moustafa, ni baada ya kututumia taarifa za kuweza kuwatumia wachezaji hao kwenye mchezo wa awali tutakaoanza kuucheza hapa nyumbani dhidi ya Pyramids.

 

“Hivyo kama uongozi tumezipokea taarifa hizo kwa mikono miwili huku tukisubiria rasmi vibali hivyo kutoka Caf.

“Sasa ni wakati mzuri wa benchi letu la ufundi kuanza kuwandaa wachezaji hao kwa kuwaingiza kwenye mipango yao katika kuelekea mchezo huo mgumu,” alisema Mwakalebela.

 

WILBERT MOLANDI, YDar es Salaam

Comments are closed.