CAF Yamchongea Luis Kwa Al Merrikh
UNAAMBIWA kitendo cha Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kulitaja bao la Luis Miquissone, kama bao bora la wiki katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, Al Merrikh wamelazimika kumfuatilia kwa ukaribu nyota huyo raia wa Msumbiji.
Nyota huyo ambaye pia ameingia kwenye kikosi bora cha wiki cha michuano hiyo baada ya kufunga bao katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Al Ahly, Jumanne ya wiki iliyopita, pia amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa wiki.
Hali hiyo imemfanya rais wa Klabu ya Al-Merrikh, Adam Sudacal kuahidi kitita cha zaidi ya dola elfu 80 (zaidi ya Sh milioni 184.9) kuwapatia wachezaji wake endapo watamzuia mchezaji huyo na kuifunga Simba.
Chanzo chetu kutoka Sudan, kimelieleza Spoti Xtra, kwamba, habari ya mjini katika Mji wa Khartoum ambapo Simba itacheza na Al Merrikh Jumamosi hii, kwa sasa ni Luis ambaye amepelekea mchezo huo kuwa na mwamko mkubwa.
“Unaambiwa mambo yameharibika Sudan, mchezo wetu na Al Merrikh utakuwa mgumu kupita mechi zote tulizocheza maana bosi wa klabu yao ameahidi zaidi ya dola elfu 80 ili watufunge.
“Mbali na hilo, tangu CAF walipotoa jina la Miquissone kuwa ndiye aliyefunga bao bora yaani mambo yameharibika kabisa kiasi kwamba gumzo lao kwa sasa ni yeye,” kilisema chanzo hicho.
STORI NA MUSA MATEJA | GPL