Na Ibrahim Mussa | CHAMPIONI |GPL
NAHODHA wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, amefunguka kuwa sababu kubwa ya kuwa na uhakika wa kutwaa ubingwa wa msimu huu, ni umoja wao licha ya kupitia kipindi kigumu cha matatizo kwenye timu yao.
Yanga ipo kileleni ikiwa na pointi 65 sawa na Simba, ikiongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City katika mchezo uliopigwa juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Cannavaro alisema haikuwa kazi rahisi kukaribia kutwaa ubingwa huo kutokana na changamoto nyingi walizopitia msimu huu ikiwa ni pamoja na kupitwa pointi nyingi na wapinzani wao Simba.
“Namshukuru Mungu, tumemaliza salama lakini mechi ya leo (juzi) ilikuwa ngumu sana kwetu, tuliambiana kabla ya mechi kama tutaweza kushinda mechi ya leo (juzi) basi sisi ndiyo mabingwa kwa kuwa ndiyo ilikuwa kizingiti kwetu na muda mwingi tulikuwa tukiifikiria.
“Safari hii ligi imekuwa ngumu lakini pia tumepitia changamoto nyingi, naamini umoja na nidhamu yetu vimetusaidia kufikia hapa licha ya kupitwa na Simba ambao leo wanatufukuzia ila sasa watake wasitake nawaambia ukweli Yanga ndiyo mabingwa na watatusamehe,” alisema Cannavaro.