Kartra

Carlinhos apelekwa hospitali fasta

TAARIFA kutoka ndani ya kambi za Yanga zinasema kuwa, Juzi Jumatatu madaktari wa kikosi hicho, walilazimika kuwakimbiza hospitali nyota wake wawili ambao ni Carlos Carlinhos na beki wao Dickson Job, lengo ni kuhakikisha wanarejea kikosini mapema kabla ya kuvaana na Simba.

 

Carlinhos aliumia kwenye mchezo wa FA, dhidi ya Prisons, mechi iliyopigwa katika Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga, wakati Job yeye aliumia wakati wa mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC.

 

Chanzo chetu kutoka ndani ya Yanga kimebainisha kwamba, juzi Jumatatu, kocha wao Nasredine Nabi alimtaka daktari wa timu hiyo Shecky Mngazija, ahakikishe anawapeleka hospitali mapema ili kujua utimamu wao, jambo ambalo alilitekeleza na baadaye kwa pamoja wakarejea kambini tayari kwa mazoezi ya jana Jumanne.

“Kikosi kiujumla kipo safi, isipokuwa tu jana timu nzima hatukufanya mazoezi ya uwanjani na badala yake tulilazimika kufanya yale ya gym, ila Carlinhos na Job wao walipelekwa hospitali kwa ajili ya vipimo zaidi na baadaye walirejea kambini na leo nadhani wataanza mazoezi ya pamoja,” kilisema chanzo hicho.

 

Championi lilimtafuta daktari wa timu hiyo, Shecky Mngazija, ambapo alisema: “Kuhusu taarifa za wagonjwa kwa sasa mimi siruhusiwi kuzungumza lolote zaidi mtafute msemaji wa timu yeye ndiye atakufafanulia zaidi kwani sisi tumezuiwa kutoa taarifa za wachezaji kwa sasa.

Stori: Musa Mateja, Dar es Salaam


Toa comment