The House of Favourite Newspapers

Carlinhos, Saido Kucheza Pamoja Dhidi ya Biashara

0

KWA mara ya kwanza, viungo washambuliaji wa Yanga, Mrundi, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ na Muangola, Carlos Fernandez ‘Carlinhos’ leo wanatarajiwa kucheza pamoja katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.

 

Yanga leo inatarajiwa kuvaana dhidi ya Biashara United katika mchezo wa ligi utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam.

 

Nyota hao tangu wajiunge na Yanga, hawajawahi kukutana na kucheza pamoja kwenye mechi za mashindano, hivyo leo kuna uwezekano mkubwa wakacheza pamoja.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Meneja Mkuu wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kuwa wachezaji hao watakutana kucheza pamoja katika mchezo wa leo dhidi ya Biashara baada ya Carlinhos kumaliza adhabu yake ya kadi nyekundu.

Saleh alisema kuwa mastaa hao hawakukutana kucheza pamoja kutokana na sababu mbili ambazo ni majeraha na adhabu ya kadi nyekundu pekee na siyo kingine.

 

Aliongeza kuwa, awali wakati Saido anajiunga na Yanga, Carlinhos alikuwa anasumbuliwa na majeraha ya kifundo cha mguu kilichomuweka nje ya uwanja kwa zaidi ya mwezi mmoja na nusu kabla ya kurejea kuitumikia timu yake.

“Carlinhos na Saido huu utakuwa mchezo wao wa kwanza kucheza pamoja kama kocha atawapa nafasi ya kuwaanzisha katika kikosi chake cha kwanza.

 

“Kwani wachezaji hao tangu wamejiunga na Yanga hawakuwahi kukutana kucheza mechi moja, hiyo imetokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya majeraha na adhabu ya kadi.

 

“Wakati Saido anajiunga na Yanga katika usajili wa dirisha dogo Carlinhos alikuwa na majeraha, alipopona anarudi uwanjani akamkuta Saido yupo katika majeraha.

 

“Na wakati Saido anapona majeraha yake, akamkuta Carlinohs yupo katika adhabu ya kadi njekundu iliyomfanya aikose michezo mitatu ambayo imemalizika mechi dhidi ya KMC, hivyo kesho (leo) watakutana kwa mara ya kwanza kucheza pamoja,” alisema Saleh.

Stori: WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave A Reply