CCM Tumewekewa Mapingamizi, Tunaamini Haki Itatendeka
_Makalla awataka wanachama katika maeneo hayo kuwa watulivu_
_Akemea vyama vya upinzani kufanya hadaa na kupotosha umma kuhusu mapingamizi_
_Asema hata CCM imewekewa mapingamizi, kinafuata taratibu_
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Itikadi Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla, amewaomba wanachama katika maeneo ambayo wagombea wa CCM wamewekewa mapingamizi, kuwa watulivu kwani Chama kinaamini haki itatendeka kwa vyama vyote.
CPA Makalla aliyasema hayo leo wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, ambapo amesisitiza CCM kitaibuka na ushindi wa haki katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.
“Niwaombe wanaCCM, tupo katika hatua za mapingamizi. Sasa hivi kinachoendelea mitandaoni ni malalamiko ya vyama vya upinzani kuonyesha kama vile pekee ndiyo waliowekewa mapingamizi.
“Wanafanya hadaa, upotoshaji wa takwimu feki na kujisahaulisha kwamba hata wagombea wa CCM wamewekewa mapingamizi. Juzi nilisema tunaamini TAMISEMI itatenda haki kwa vyama vyote kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki na atakayeshinda atangazwe kwa haki,” alisema Makalla na kusisitiza:
“Kwa hesabu zetu na wagombea tuliowaweka, tunaamini CCM tutashinda kwa haki. Kwa hiyo rufaa zinaendelea, baada ya uteuzi wa wagombea CCM kitatoa taarifa baadaye.”
CPA Makalla alikemea tabia hiyo ya baadhi ya vyama vya upinzani kupotosha umma kwamba wagombea wa vyama hivyo pekee, ndiyo wamewekewa mapingamizi, wakati si kweli.
Alisema kuwa vyama vyote, kikiwemo CCM, ambavyo wagombea wake wamewekewa mapingamizi ya kuteuliwa, vinaendelea kukata rufaa, kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Niwaombe wanaCCM katika maeneo ambayo tumewekewa mapingamizi, tuwe watulivu tukiamini haki itatendeka kwa vyama vyote,” alisisitiza CPA Makalla.